Dec 05, 2023 09:28 UTC
  • Vladimir Putin
    Vladimir Putin

Rais wa Russia amesema, mzozo wa muda mrefu katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu umefikia hali ya maafa halisi ya binadamu.

Rais wa Russia, Vladimir Putin, alisema jioni ya jana Jumatatu kwamba: "Uhusiano wa kimataifa uko katika wakati mgumu sana ambapo migogoro ya kisiasa na kiuchumi imeongezeka duniani."

Putin pia ameongeza kuwa Russia iko tayari kushirikiana kwa karibu na nchi zote marafiki kutatua matatizo muhimu ya kikanda na kimataifa.

Hivi karibuni, katika ujumbe wake kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina, Rais wa Russia alieleza kuwa, kuundwa kwa taifa huru la Palestina kwa kuzingatia mipaka ya mwaka 1967 ni moja ya masharti makuu ya kuanzisha amani ya kudumu na ya kiadilifu kati ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Gaza

Hapo awali, Dmitry Chumakov, naibu mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, alivitaja vita vya Gaza kuwa ni "mgogoro wa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa", na kusema kuwa hatari ya kupanuka kwake inatishia eneo lote la Asia Magharibi.

Ndege za kivita, mizinga na askari wa nchi kavu wa jeshi la Kizayuni wanaendele kuyashambulia maeneo ya kusini mwa Gaza hususan Khan Yunis kwa mabomu ya fosforasi.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina, idadi ya mashahidi wa Kipalestina tangu kuanza kwa vita vya Kimbunga cha Al-Aqsa (Oktoba 7) imefikia 15,899 na wengine 42,000 wamejeruhiwa. Zaidi ya nusu ya waliouawa ni wanawake na watoto wadogo.

Tags