Iran yajibu bwabwaja, vitisho na matamshi ya uingiliaji ya Trump
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameonya kwamba, uingiliaji kati wa Marekani katika masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu utavuruga utulivu wa eneo zima la Asia Magharibi na kuhatarisha moja kwa moja maslahi ya Marekani katika eneo.
Ali Larijani amesema hayo katika ujumbe alioutuma leo kwenye mtandao wa kijamii wa X na kueleza kwamba, misimamo ya hivi karibuni iliyochukuliwa na maafisa wa Israel na Rais wa Marekani, Donald Trump imeanika njama za nyuma ya pazia juu ya matukio ya sasa nchini.
Amesisitiza kwamba, Iran inatofautisha wazi kati ya wamiliki wa biashara wanaoandamana kwa amani hapa nchini na waharibifu wanaotaka kutumia vibaya maandamano hayo, akisisitiza kwamba uingiliaji kati wa kigeni utabadilisha kimsingi hali hiyo.
Katika ujumbe wa moja kwa moja, afisa huyo mwandamizi wa Iran ameongeza kwamba, umma wa Marekani unapaswa kuelewa kwamba ni Trump aliyeanzisha uvamizi, akiwaonya waangalie usalama wa wanajeshi wa Marekani.
Rais wa Marekani Donald Trump leo Ijumaa ametoa vitishio vipya dhidi ya Iran, akidai kwamba Washington "imejiandaa barabara" na iko tayari kuingilia kati iwapo mamlaka ya Iran itadaiwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameonya kwamba, Trump anapaswa kufahamu kikamilifu kwamba kuhusika kwa Marekani katika suala la ndani kungesababisha ukosefu wa utulivu wa kikanda na mmomonyoko wa maslahi ya Marekani.
Katika ujumbe kwenye jukwaa lake la Truth Social, Trump amebwabwaja kwamba: Ikiwa Iran "itawapiga risasi na kuwaua waandamanaji wa amani," Marekani "itawaokoa."
Kauli ya Trump inafuata mkumbo maarufu, ambapo maafisa wa Marekani hujinadi kama watetezi wa haki za binadamu nje ya nchi, huku wakipuuza au kuhalalisha majibu makali ya vyomvo vya dola dhidi ya wapinzani na wakosoaji ndani ya Marekani kwenyewe.