May 10, 2024 02:11 UTC
  • Iran yakosoa vitisho na mashinikizo wawakilishi wa Kongresi dhidi ya mahakama ya ICC

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa ni fedheha na jambo lenye kutia wasiwasi kuona baadhi ya wawakilishi wa Kongresi na Seneti ya Marekani wanatoa vitisho na kuwashinikiza waendesha mashtaka na majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Nasser Kan'ani ameandika katika ukurasa wake wa mtandao kijamii wa X kwamba lengo la kundi la wawakilishi wa Kongresi na Seneti ya Marekani ni kuwatishia na kuwashinikiza waendesha mashtaka na majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ili kutoa kinga kwa maafisa na makamanda wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliofanya jinai za kivita na mauaji ya kimbari huko Gaza. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameitaja hatua hii kuwa ni fedheha na yenye kutia wasiwasi.  

Wawakilishi na Maseneta 12 wa Marekani walioitishia ICC 

Kan'ani ameeleza kuwa, kuingilia kazi za waendesha mashtaka na majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutaibua utaratibu hatari ambao ni kinyume na malengo na falsafa ya uwepo wa mahakama hiyo wa kuwaadhibu watenda jinai za kivita.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema pia kuwa kimya cha jamii ya kimataifa mkabala wa vitsho hivyo kinazuia kutekelezwa uadilifu na badala yake jinai dhidi ya wananchi wa Palestina zitaendelea.   

Wabunge kadhaa wa chama cha Republican nchini Marekani wametangaza kuwa watawasilisha sheria ya adhabu na kuiwekea vikwazo vikali mahakama ya Umoja wa Mataifa ya ICC iwapo  itatoa waranti wa kutiwatia nguvuni viongozi wa utawala wa Israel wanaotuhumiwa kufanya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza. 

Tags