May 09, 2024 13:26 UTC
  • Vladimir Putin
    Vladimir Putin

Rais Vladimir Putin wa Russia, amesisitiza kwa mara nyengine kwamba nchi yake haitaruhusu vitisho vya aina yoyote kutoka nchi za Magharibi na kwamba vikosi vya kistratijia vya nyuklia vitaendelea kuwa tayari kutumia silaha za nyukilia.

Raisi Putin ameyasema hayo leo wakati wa gwaride la kuadhimisha Siku ya Ushindi wa nchi yake dhidi ya Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Amesema: "Russia itafanya kila iwezalo kuepusha makabiliano ya kimataifa, lakini wakati huo huo hatutaruhusu mtu yeyote kututishia."

Vilevile amewapongeza wanajeshi wa nchi yake wanaopigana huko Ukraine na amezituhumu nchi za Magharibi kwa kuchangia katika mizozo inayoshuhudiwa duniani.

Rais Putin ameendelea kusisitiza kuwa, vita vinayoendelea sasa nchini Ukraine ni vita vya Russia dhidi ya utawala wa kinazi.

Sherehe na gwarida kubwa limefanyika leo Red Square katika mji mkuu, Moscow, mbele ya viongozi kadhaa wa nchi za kigeni katika kumbukumbu ya miaka 79 ya ushindi wa Umoja wa Kisovieti dhidi ya Ujerumani ya Kinazi katika Vita vya Pili vya Dunia, ambavyo ilisalimu amri Mei 8, 1945.

Gwaride la Siku ya Ushindi, Moscow

Umoja wa Kisovieti ulipoteza watu milioni 27 katika Vita vya Pili vya Dunia, lakini hatimaye vikosi vya majeshi ya Kinazi yalilazimika kurudi Berlin, ambapo Adolf Hitler alijiua. Bendera nyekundu ya ushindi wa Soviet iliinuliwa juu ya jengo la Bunge la Ujerumani, Reichstag, mnamo 1945.

Sherehe ya leo ya kumbukumbu ya ushindi wa Umoja wa Sovieti dhidi ya Ujerumani ya Kinazi imefanyika huku uhusiano wa Russia na nchi za Magharibi ukiendelea kusuasua kutokana na kusonga mbele kwa vikosi vya Russia dhidi ya vikosi vya Ukraine vinavyoungwa mkono na nchi za Magharibi.