May 09, 2024 02:24 UTC
  • Mashambulizi ya Israel dhidi ya Rafah: Sababu na matokeo yake

Katika hali ambayo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetangaza kukubaliana na mpango wa usitishaji vita wa Misri na Qatar, utawala wa Kizayuni wa Israel umezidisha mashambulizi makali dhidi ya mji wa Rafah huko Ukanda wa Gaza.

Zaidi ya miezi 7 sasa imepita tangu Israel ianzishe vita na mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa Gaza. 

Gaza

Harakati ya Hamas imeonyesha nia nzuri ya kufikia makubaliano ya kumaliza vita, lakini makadirio yanaashiria kuwa, utawala wa Kizayuni unapanga kupanua vita na kufanya mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imetangaza kwamba: "Baraza la Mawaziri la Vita  limeamua kwa kauli moja kuendeleza operesheni zake huko Rafah ili kutimiza malengo yetu ya kukomboa mateka na malengo mengine ya kivita kupitia njia ya kuzidisha mashinikizo ya kijeshi dhidi ya Hamas.

Msemaji wa jeshi la utawala wa Kizayuni alitangaza jana Jumanne kwamba, jeshi la utawala huo limetwaa sehemu ya Palestina ya kivuko cha mji wa Rafah.

Wakati huo huo, msemaji wa Bodi ya Vivuko vya Ukanda wa Gaza ametangaza kuwa: Utawala haramu wa Israel umewahukumu kifo wakazi wa Gaza baada ya kufunga kivuko cha mji Rafah kinachopitisha misaada kwa ajili ya Wapalestina.

Inaonekana kuwa, sisitizo la utawala wa Kizayuni la kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji wa Rafah na wakazi wake linatokana na mambo matatu.

Kwanza ni kwamba, baraza la mawaziri la Netanyahu linaundwa na watu wenye hitilafu na tofauti za kifikra, kitabia na kitaaluma. Kwa sababu hii tunaona kuwa, wakati baadhi ya wajumbe wa baraza la mawaziri la Netanyahu wakisisitiza ulazima wa kusitishwa mapigano, watu wengine kama vile Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala haramu wa Israel, wanatishia kuondoka kwenye baraza la mawaziri iwapo jeshi halitaushambulia mji wa Rafah.

Netanyahu na Ben-Gvir

Pili ni kuwa, Benjamini Netanyahu anaona kuwa anapaswa kuendeleza vita ili aendelee kuweko madarakani. Kuhusiana na jambo hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, Ayman al-Safadi, amekosoa uamuzi wa utawala wa Israel wa kuishambulia Rafah na kusema kuwa, Netanyahu anataka kupanua vita ili kulinda mustakabali wake wa kisiasa.

Jambo la tatu ni kuwa, utawala wa Kizayuni unaona kwamba, kusitishwa vita bila ya kufikia malengo yake muhimu ikiwa ni pamoja na kuiangamiza Hamas kuna maana ya kushindwa vitani na kufeli madai yake ya kijeshi na kijasusi. Kwa msingi huo, anasisitiza chaguo la kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji wa Rafah, katika jaribio la kupata pointi na kujiweka katika nafasi bora mkabala wa Hamas katika meza ya mazungumzo.

Jambo lenye muhimu ni kwamba, mashambulizi makubwa dhidi ya mji wa Rafah yatasababisha hali mbaya kwa Ukanda wa Gaza na mji wa Rafah ambao kwa sasa umewapa hifadhi mamia ya maelfu ya Wapalestina.

Kuwepo kwa vikosi vya jeshi la Israel katika kivuko cha Rafah kumepelekea kufungwa kivuko hicho na kuwazuia Wapalestina kusafiri kupitia eneo hilo. Kufungwa kivuko hicho cha mpakani pia kutawaweka wagonjwa wa Kipalestina katika makucha na meno ya mauti katika mazingira ya sasa ya kuporomoka kwa mfumo wa afya wa Ukanda wa Gaza.

 Kwa msingi huo inatupasa kusema kuwa, shambulio la Israel dhidi ya Rafah ni kushindwa kwingine kwa jamii ya kimataifa katika kukomesha mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa Gaza na kunazidi kuporomosha chini hadhi jamii ya kimataifa hasa Umoja wa Mataifa.