May 09, 2024 02:30 UTC
  • Mawakili wa Uholanzi waitaka ICC itoe waranti wa kukamatwa Netanyahu

Kundi la mawakili wa Uholanzi wameiomba Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutoa waranti wa kumtia nguvuni Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza.

Televisheni ya al-Jazeera imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wataalamu hao wa sheria wa Uholanzi wameitaka ICC kuharakisha mchakato wa kutiwa nguvuni Netanyahu na maafisa wengine wa Israel, mara tu itakapotoa vibali vya kukamatwa watenda jinai hao.

Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth, limemnukuu afisa mmoja wa utawala haramu wa Israel akisema kuwa kuna uwezekano ICC itatoa kwa siri waranti wa kukamatwa maafisa wa Israel. 

Hii ni katika hali ambayo, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa ICC imetoa wito wa kusitishwa vitisho kwa wafanyakazi wa mahakama hiyo, ikisema kuwa vitisho hivyo vinaweza kuwa uhalifu dhidi ya korti hiyo inayoshughulikia uhalifu wa kivita.

Makahama ya ICC yenye makao yake mjini Hague, Uholanzi

ICC imetoa tamko hilo baada ya Israel na Marekani kukosoa uchunguzi unaofanywa na mahakama hiyo ya kimataifa kuhusu madai ya uhalifu wa kivita uliofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.

Viongozi wa Marekani wameanzisha kampeni kubwa ya kuzuia hatua yoyote ya mahakama hiyo ya kimataifa kutoa kibali cha kukamatwa viongozi watenda jinai na mauaji ya kimbari wa Israel, hususan Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya binadamu. 

Tags