Iran: Vikwazo vya US dhidi ya majaji wa ICC vinakirihisha
(last modified Mon, 09 Jun 2025 02:49:38 GMT )
Jun 09, 2025 02:49 UTC
  • Iran: Vikwazo vya US dhidi ya majaji wa ICC vinakirihisha

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei amekosoa vikali hatua ya Marekani ya kuwawekea vikwazo majaji wanne wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutokana na uchunguzi wao juu ya uhalifu wa kivita uliofanywa na Israel huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Baqaei amesema vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya majaji wanne wa ICC vinafedhehesha na  kutia kichefuchefu. Siku ya Alkhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio alitangaza kuwa majaji 4 wa ICC wameongezwa kwenye orodha ya vikwazo, akiwatuhumu kukiuka mamlaka ya Marekani na Israel.

"Kuwekewa vikwazo majaji na wafanyakazi wa ICC ni jambo la kuchukiza na kufedhehesha sana, hata kwa mfumo ambao una uraibu wa kuendeleza sera yake ya kigeni kupitia vitisho," Baqaei amesema kupitia ujumbe aliotuma kwenye akaunti yake ya X.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema Marekani inatumia vibaya mamlaka yake katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupinga maazimio ya kutaka kusitishwa mauaji ya kimbari huko Gaza ili kuhakikisha kwamba Israel haiwajibishwi kwa mauaji ya halaiki ya Wapalestina.

Amesema vitendo hivyo vimeifanya Marekani kuwa mshirika katika mauaji ya halaiki, jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu na vitendo vya uchokozi vinavyofanywa na utawala ghasibu wa Israel na kusisitiza kuwa, umefika wakati kwa jamii ya kimataifa kusimama kidete kukabiliana na ukatili huo ambao unadhoofisha haki za kimataifa na kanuni za kibinadamu.

Kabla ya hapo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk alisema "amesikitishwa sana" na vikwazo hivyo vya serikali ya Marekani dhidi ya majaji wanne wa ICC.