Papa Leo achukua hatua ya kwanza kushughulikia ubakaji wa makasisi
-
Papa Leo XIV
Papa Leo XIV Jumamosi ya jana alimteua Askofu Mkuu wa Ufaransa kuwa mkuu mpya wa tume ya Vatican kuhusu unyanyasaji wa kingoni unaofanywa na makasisi, ikiwa ni hatua yake ya kwanza ya wazi ya kushughulikia suala ambalo limeharibu hadhi na taswira ya Kanisa Katoliki duniani.
Thibault Verny, 59, atakuwa mkuu wa Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto, lakini atabaki kuwa askofu mkuu wa Chaubéry kusini mashariki mwa Ufaransa.
Verny amesema amejitolea kuboresha ulinzi ndani ya kanisa, na kuongeza katika taarifa yake kwamba: "Tutafanya kazi kukuza ugawaji sawa wa rasilimali ili sehemu zote za kanisa, bila kujali jiografia au hali, ziweze kudumisha viwango vya juu zaidi vya ulinzi."
Papa aliyeaga dunia karibuni, Francis alianzisha tume hiyo mwaka 2014 katika jaribio la kukabiliana na kashfa za unyanyasaji wa kingono zilizotikisa Kanisa Katoliki kote duniani.
Kashfa hizo zimeharibu sana sura ya Kanisa kama sauti ya maadili, na kuibua kesi za mamilioni ya dola sambamba na kupelekea kujiuzulu kwa maaskofu kadhaa.
Papa Francis, aliyeaga dunia April 21, 2025 aliwahi kukiri mara kadhaa kwamba, kanisa hilo linakabiliwa na mgogoro wa udhalilishaji wa kingono, huku makasisi na maaskofu wa kanisa hilo wakiwafanya watawa watumwa wa ngono.

Kuna mamia ya kesi za ubakaji na ulawiti zinazowakabili makasisi na viongozi wengine wa kanisa hilo, ambazo zimerundikana katika mahakama za Ulaya na Marekani zikisubiri kufanyiwa uchunguzi, jambo ambalo limeshusha hadhi ya Kanisa Katoliki duniani.