May 08, 2024 07:15 UTC
  • Ebrahim Raisi: Iran yenye nguvu ina uwezo wa kuondoa chaguo la kijeshi kwenye meza ya adui

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Operesheni ya "Ahadi ya Kweli" ilileta fahari ya kitaifa na akaielezea kuwa ni dhihirisho la wazi kabisa la mantiki ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Rais Ebrahim Raisi amesisitiza kwamba Iran yenye nguvu ina uwezo wa kuondoa chaguo la kijeshi kwenye meza ya adui.

Akizungumzia operesheni ya kijeshi ya Iran ya Ahadi ya Kweli iliyokuwa jibu dhidi ya shambulio la Israel katika ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus Syria, Rais amesema, wigo wa operesheni hiyo unapaswa kujadiliwa na kutafitiwa katika mikutano mbalimbali ya kisayansi, kiutafiti, kisiasa na kiusalama.

Raisi ameelezea Operesheni Ahadi ya Kweli kuwa ni chimbuko la fahari ya taifa na kusema: Kila mtu alisifu operesheni hii, ambayo inaweza kupelekea kutatua matatizo, kujenga maelewano, na fahari ya kitaifa katika maeneo mengine.

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Rais wa Iran amesema pia kuwa, utawala wa  Kizayuni wa Israel umekata tamaa na umeshindwa, na moja ya madhihirisho ya kukata tamaa ni shambulio dhidi ya ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus, Syria kitendo ambacho kinakiuka sheria na kanuni zote za kimataifa.

Ebrahim Raisi amebainisha kwamba, Gaza ni dhihirisho la kuelimika, muqawama, kutotetereka, uthabiti, subira na upendo wa Mungu na kwa mujibu wa wataalamu wote wa masuala ya kisiasa duniani, mshindi katika uwanja huo ni watu wa Palestina waliosimama imara na kidete, na mwenye kushindwa katika uwanja huo ni utwala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake.