May 10, 2024 02:58 UTC
  • Chad yamtangaza Deby kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais, upinzani wapinga

Tume ya Uchaguzi nchini Chad imemtangaza Mahamat Idriss Deby Itno, Rais wa serikali ya mpito na kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo, kuwa mshindi halali wa uchaguzi wa rais uliofanyika siku chache zilizopita.

Mkuu wa Wakala wa Kitaifa wa Kusimamia Uchaguzi Chad, Ahmed Bartichet alitangaza jana Alkhamisi kuwa, Deby ndiye mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Mei 6, baada ya kuzoa asilimia 61.3 ya kura zilizopigwa, katika hali ambayo, mgombea mkuu wa upinzani, Succes Masra amejitangaza pia kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya Chad, Masra mwenye umri wa miaka 40, na Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya nchi hiyo, ameambulia asilimia 18.53 ya kura.

Aidha wagombea wengine wa upinzani nchini humo wamepinga matokeo hayo yaliyotangazwa jana Alkhamisi na Wakala wa Kitaifa wa Kusimamia Uchaguzi Chad, wakisisitiza kuwa uchaguzi huo uligubikwa na mizingwe na uchakachuaji wa matokeo.

Uchaguzi wa rais uliofanyika Jumatatu wiki hii unakusudiwa kuhitimisha miaka mitatu ya utawala wa kijeshi huko Chad. Hata hivyo wapinzani wa mtawala wa kijeshi wa nchi hiyo walitoa wito wa kususia uchaguzi wakisema kuwa matokeo tayari yameshapangwa.

Mgombea mkuu wa upinzani Chad aliyepinga matokeo, Succes Masra

Hapo awali chama cha The Transformers cha mpinzani mkuu wa rais wa serikali ya mpito ya Chad kilidai kuwa kimezuiwa kufika katika vituo vya kupigia kura ili kushuhudia zoezi la kuhesabu kura. 

Hali ya taharuki imetanda nchini humo, huku wadadisi wa mambo wakionya kuwa, huenda taifa hilo likatumbukia katika ghasia za baada ya uchaguzi.

Deby ambaye aliwania urais kwa tiketi ya chama tawala cha Patriotic Salvation Movement (MPS), alichukua mamlaka mnamo Aprili 2021 baada ya kifo cha baba yake, Idriss Deby Itno, ambaye aliuawa kwenye mstari wa mbele wa vita dhidi ya waasi baada ya kutawala kwa miaka 30.