May 02, 2024 02:35 UTC
  • Jitihada za China za kuleta maridhiano ya kitaifa Palestina

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ametangaza kuwa kufuatia mkutano wa wawakilishi wa harakati za Palestina za Hamas na Fat'h mjini Beijing, pande mbili zimefikia makubaliano ya kujadili maridhiano ya kitaifa huko Palestina.

Kwa mujibu wa Lin Jian, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, wawakilishi wa harakati za Palestina za Fat'h na Hamas wamefanya mashauriano mjini Beijing na kusisitiza nia yao ya kuendeleza mazungumzo na kufikia umoja wa Palestina. Kwa hakika pande zote mbili zimeonyesha nia ya kuendelea na mazungumzo ili kufikia mshikamano na umoja wa Wapalestina. Hatua ya China ya kukaribisha makundi ya Wapalestina ili kuleta maelewano na maridhiano ya kitaifa ni ishara ya kuwa Beijing ina nafasi chanya katika kuleta maelewano katika eneo la Asia Magharibi.

Katika miaka ya nyuma, China ilipendelea kuzingatia masuala yake ya ndani, ikiwa ni pamoja na kuendelea kwa ukuaji wa uchumi, bila kujihusisha moja kwa moja na masuala ya kieneo.

Mohsen Ruuyi Sefat, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema hivi kuhusu muelekeo mpya wa China:

 "China, ikiwa mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, haijakuwa na nafasi muhimu ya kisiasa au kidiplomasia katika ngazi ya kikanda na kimataifa. Lakini tangu miaka michache iliyopita, mtazamo wa kisiasa wa serikali ya Beijing umebadilika."

Nukta hii inaonyesha kwamba Beijing imedhamiria kuchukua nafasi ya kisiasa inayolingana na hadhi yake ya kimataifa, na inatarajiwa kuwa itakuwa na nafasi inayozidi kuimarika katika masuala ya Asia Magharibi.

Ukweli ni kwamba kwa mtazamoa wa kihisotria, China imekuwa muungaji mkono wa malengo ya ukombozi wa Palestina lakini hadi sasa, haijachukua hatua zozote za maana katika kutatua kadhia ya Palestina. Hata wakati huu wa mauaji ya kimbari yanayoendelezwa na utawala wa Isarel huko Gaza, jamii ya kimataifa ilitarajia Beijing ichukue hatua muhimu na za kivitendo kwa ajili ya kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni lakini haikuchukua hatua ilivyotarajiwa bali imetosheka tu kwa kuunga mkono mtazamo wa nchi za Kiarabu na Kiislamu katika uwanja huo.

Kwa mfano, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alisema mnamo Aprili 18 kwamba Marekani inapaswa kuunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa la kuanzisha usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza. Alisisitiza kuhusu takwa la Beijing la "kusitishwa mara moja mapigano". Aidha aliviita vita vya Israel dhidi ya Gaza kuwa ni janga.

Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China

Mwakilishi wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, Zhang Jun, pia alisisitiza haja ya kusimamishwa mashambulizi ya Gaza na kukomeshwa kudhuriwa raia.

Wakati huo huo wakazi wa Ukanda wa Gaza na wapigania uhuru wa dunia wamekuwa wakitarajia kuwa China itachukua hatua imara zaidi za kivitendo kuulazimisha utawala wa Kizayuni usitishe mauaji ya kimbari huko Gaza. Hakuna shaka kuwa muendelezo wa mauaji ya kimbari ya watu wa Gaza, ambapo hadi sasa makumi ya maelfu wameuawa shahidi, ni jambo ambalo linaumiza moyo wa kila mtu aliye huru duniani.

Kwa hiyo, ingawa China kuwa mwenyeji wa makundi ya Palestina Hamas na Fat'h ni nukta chanya na muhimu kwa umoja wa kitaifa wa Palestina lakini hatua hiyo haitoshi. China, kama mjumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, bila shaka inaweza kuwa na ufanisi muhimu zaidi katika kukomesha jinai za Wazayuni huko Gaza. 

Ulimwengu bila shaka unatarajia nchi kama China kuwa na nafasi zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake katika kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu Gaza wasio na hatia.

Tags