May 14, 2024 10:25 UTC
  • UNICEF yataka kukomeshwa mauaji ya watoto yanayofanywa na Israel Gaza

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetoa mwito wa kukomeshwa mauaji ya kiholela dhidi ya Wapalestina, hasa watoto wadogo katika Ukanda wa Gaza.

Katika mahojiano na shirika la habari la ABC la Marekani, Msemaji wa UNICEF, Tess Ingram ametoa mwito wa kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza, huku akitahadharisha kuhusu taathira hasi za za hujuma za utawala vamizi wa Israel huko Gaza, ukiwemo mji wa kusini wa Rafah.

Amesema, wakati wa ziara yake huko Gaza, na hasa mjini Rafah, alishuhudia taswira za kuogofya za watoto waliolazwa hospitalini bila kutibiwa, kutokana na athari za vita hivyo.

Ingram amesilimua kwa kusema, "Niliona mtoto wa miaka 9 ambaye alikuwa amelazwa hospitalini akiwa katika hali mahututi, upande mmoja wa mwili wake ulikuwa na majeraha yaliyotokana na shambulizi kubwa. (Mtoto huyo) alisema amekuwa katika hali hiyo (ya uchungu na maumivu) kwa siku 16, kwa kuwa mfumo wa matibabu wa Gaza hauwezi kumtibu majeraha hayo."

"Tunataka kuona mapigano na mauaji ya kiholela ya raia, hasa watoto yakifikia tamati," ameongeza Msemaji wa UNICEF, Tess Ingram katika mahojiano na kanali ya ABC.

Vyanzo rasmi vya habari vimeripoti kuwa, katika kila dakika 10, mtoto mmoja huuawa au kujeruhiwa katika mashambulizi ya kinyama ya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa UNICEF, watoto karibu 15,000 wa Kipalestina ni miongoni mwa watu zaidi ya 35,000 waliouawa hadi sasa katika mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza huko Palestina tokea Oktoba 7, 2023.

Tags