UN: Tuna wasiwasi kutokana na kushtadi mapigano, taharuki Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128400
Wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema wana wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka kwa mapigano nchini Sudan, hasa mashambulizi ya karibuni katika Jimbo la Kordofan Kaskazini.
(last modified 2025-07-17T02:48:31+00:00 )
Jul 16, 2025 12:41 UTC
  • UN: Tuna wasiwasi kutokana na kushtadi mapigano, taharuki Sudan

Wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema wana wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka kwa mapigano nchini Sudan, hasa mashambulizi ya karibuni katika Jimbo la Kordofan Kaskazini.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema mashambulizi yaliyoanzia Aklhamisi hadi Jumapili kwenye vijiji karibu na mji wa Bara huko Kordofan Kaskazini yaliripotiwa kuua takriban watu 300, wakiwemo watoto na wanawake wajawazito.

Mbali na vifo, watu wengine zaidi walijeruhiwa, na nyumba kuporwa na kuchomwa moto, huku watu wakikimbia makazi, shirika la habari la Xinhua limeripoti. OCHA imesema kukatika kwa mawasiliano kunazuia juhudi za kuthibitisha idadi kamili ya waliouawa na kujeruhiwa. 

Ofisi hiyo ya UN pia imesema imesikitishwa na ripoti za mashambulizi mapya ya makombora huko El-Obeid, mji mkuu wa jimbo hilo. "Shambulio hilo linazidisha hofu na ukosefu wa usalama." imesisitiza OCHA.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu imesisitiza kuwa, raia na miundombinu ya kiraia, zikiwemo shule, nyumba, makazi na mali za kibinadamu, kamwe hazipaswi kulengwa, na kutoa wito kwa pande zote kwenye mzozo kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu kikamilifu.

Kundi la kutetea haki za binadamu la ‘Wanasheria wa Dharura’ lilisema katika taarifa yake Jumatatu kwamba, RSF imeshambulia vijiji kadhaa tangu Jumamosi iliyopita karibu na mji wa Bara, ambao wanamgambo hao wanaudhibiti na kuua watu zaidi ya 300.

Jimbo la Kordofan Kaskazini limekuwa likishuhudia ongezeko la mashambulizi tangu mapigano makali kati ya jeshi la kitaifa la Sudan na waasi wa RSF yalipozuka mwezi Aprili 2023.