May 26, 2024 13:18 UTC
  • Maandamano ya kuitetea Palestina yashuhudiwa Ulaya licha ya vizingiti

Miji na majiji makubwa ya Ulaya jana Jumamosi yalishuhudia maandamano ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, sanjari na kutaka kusitishwa mara moja vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya eneo hilo lililozingirwa.

Huko Berlin, mji mkuu wa Ujerumani,  maelfu ya watu walijitokeza mabarabarani kuandamana katika mji huo kuonyesha mshikamano kwa wananchi wa Palestina, licha ya kuwekewa mbinyo na vyombo vya usalama.

Waandamanaji jijini Berlin huku wakiwa na mabango yaliyoandikwa 'Kamwe Palestina haitokufa',  walisikika wakipiga nara na shaari kama "Palestine iwe huru, vita visitishwe sasa, na acha mauaji ya kimbari."

Wafanya maandamano huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa walikusanyika nje ya Kanisa Katoliki la Montmartre Sacré-Coeur kuitetea Palestina. Huku wakiwa wamebeba bendera za Palestina, walisikika wakipiga nara na kutoa wito wa kusitishwa vita na mashambulizi ya mabomu ya Israel dhidi ya Gaza.

Polisi katika nchi za Ulaya wanavyokandamiza maandamano ya amani

Aidha Stockholm, mji mkuu wa Sweden pia ulishuhudia maandamano ya kutaka kusitishwa vita na mashambulizi ya mabomu ya Israel dhidi ya Gaza. Kadhalika wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dublin nchini Ireland jana waliendeleza maandamano ya kuliunga mkono taifa la Palestina na kutaka kusitishwa mauaji ya kimbari Gaza.

Hapo jana pia, Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya alisema EU inapasa kuweka bayana msimamo wake kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) wa kuutaka utawala wa Israel usitishe mara moja mashambulizi yake ya kijeshi mjini Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa, EU inapasa kuchagua ama kuunga mkono taasisi za kimataifa na utawala wa sheria, au kuingaji mkono Israel.

Utawala wa Kizayuni unaendesha vita na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7 mwaka jana; ambapo hadi sasa umewaua shahidi Wapalestina zaidi ya 35,000 na kujeruhi zaidi ya 80,000.

Tags