Mwangwi wa shambulizi la kigaidi la Nice
Shambulizi la kigaidi lililofanyika jana usiku katika mji wa pwani wa Nice nchini Ufaransa limeacha mwangwi mkubwa katika pembe mbalimbali za dunia.
Watu wasiopungua 84 wameuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika shambulizi hilo la kigaidi ambalo ni la tatu kubwa kutokea nchini Ufaransa katika kipindi cha miaka miwili ya hivi karibuni.
Baada ya shambulizi hilo nchi jirani na Ufaransa ikiwemo Italia, Uhispania na Ujerumani zimezidisha ulinzi katika mipaka yao. Rais François Hollande wa Ufaransa amesema baada ya shambulizi hilo kwamba nchi yake imepata pigo kubwa na kwamba inapaswa kufanya kila iwezalo kukabiliana na mashambulizi kama hayo. Amesema Ufaransa nzima inakabiliwa na tishio la ugaidi. François Hollande amesisitiza kuwa baada ya shambulizi la Nice, Ufarasna itazidisha mashambulizi yake katika nchi za Syria na Iraq dhidi ya ugaidi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyosababisha vifo katika mji wa Nice nchini Ufaransa.
Bahram Qasimi ameeleza kusikitishwa na mashambulizi hayo ya kigaidi na kusisitiza kuwa ugaidi hauwezi kutokomezwa iwapo hakutakuwepo ushirikiano na jitihada za kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa upuuzaji wowote na mienendo ya kindumakuwili katika kukabiliana na igaidi, inapaswa kulaumiwa.
Chuo Kikuu cha al Azhar nchini Misri pia kimetoa taarifa kikitaka kuwepo umoja na mshikamano duniani kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi.
Taarifa ya Chuo al Azhar pia imesema kuwa shambulio hilo la kigaidi linakinzana na mafundisho ya Uislamu na kusisitzia udharura wa kuunganisha juhudi kimataifa ili kuutokomeza ugaidi.
Rais Barack Obama wa Marekani pia amekemea shambulizi ya kigaidi la Nice na kutoa pendelezo la msaada wa uchunguzi wa tukio hilo kwa viongozi wa serikali ya Paris. Obama amelitaja tukio hilo kuwa ni shambulizi la kutisha la kigaidi.
Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau ni miongoni mwa viongozi wa nchi mbalimbali waliotuma salamu za rambirambi kwa taifa na serikali ya Ufaransa kutokana na shambulizi hilo la kigaidi. Amesema Wacanada wameshtushwa sana na shambulizi la Nice.
Mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk ametoa taarifa akieleza kushtushwa na kitendo cha kushambuliwa Ufaransa katika siku ya taifa ya nchi hiyo. Amesema viongozi wote duniani wanaungana na Wafaransa katika maafa hayo.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limelaani vikali shambulizi la kigaidi la Nice na kusema ugaidi ni miongoni mwa vitisho vikubwa dhidi ya amani na usalama wa kimataifa.
Msemaji wa Vatican, Federico Lombardi amesema Vatican inalaani vikali mienendo kama hiyo ya kiendawazimu, ya kuchukiza, ya kigaidi na mashambulizi mengine yote yanayolenga amani ya kimataifa.
Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang amekemea vikali shambulizi hilo la kigaidi la kusema, Beijing itapambana na aina zote za igaidi. Vilevile ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa shambulizi hilo.
Rais wa India Pranab Mukherjee amesema kuhusu shambulizi la Nice kwamba nchi yake itaimarisha ushirikiano wake na Ufaransa na nchi nyingine duniani katika vita vya kupambana na ugaidi.
Kwa upande wake Rais Vladimir Putin wa Rusia ametangaza baada ya shambulizi la jana usiku mjini Nice kuwa njia pekee ya kupambana ipasavyo na shari ya ugaidi unaoendelea kupanuka zaidi duniani ni kukomesha vipimo vya kindumakuwili na kupambana kwa nguvu zote na magaidi. Rais wa Russia amesisitiza kuwa, shambulizi la Nice limeonesha kwamba, kuna udharura mkubwa wa kupambana na ugaidi katika pande zote.