Muendelezo wa maandamano dhidi ya Wazayuni katika maeneo mbalimbali ulimwenguni
Maandamano bado yanaendelea katika nchi tofauti za dunia kupinga mauaji ya halaiki yanayofanywa na jeshi katili la utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza.
Jana Jumatano, watu wa Jordan walifanya maandamano karibu na ubalozi wa utawala ghasibu wa Israel huko Amman mji mkuu wa nchi hiyo wakilaani jinai na mauaji ya kimbari ya utawala wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu, huko katika Ukanda wa Gaza.
Televisheni ya Al-Aqsa imesema kwamba maandamano mengine makubwa yamefanyika huko Ottawa mji mkuu wa Kanada kama sehemu ya harakati zinazoendelea za kuwaunga mkono watu wa Ukanda wa Gaza unaozingirwa na utawala haramu wa Israel.
Kanali ya Telegram ya "Palestine Huru" imeripoti kwa kuchapisha video kwamba waungaji mkono wa watu wa Palestina wamelaani jinai za utawala katili wa Israel huko Gaza kwa kufanya maandamano makubwa katika mitaa ya Luxembourg.

Kanali ya Telegram ya "Palestine Online" pia imetangaza katika ripoti kwamba idadi kubwa ya waungaji mkono wa watu wa Palestina wamekusanyika katika mitaa ya Paris mji mkuu wa Ufaransa kuonyesha mshikamano wao na watu wa Palestina na kulaani jinai za Wazayuni dhidi ya watu hao wasio na hatia wala ulinzi katika Ukanda wa Gaza.
Maelfu ya Waswedi pia wamemiminika katika mitaa ya Gothenburg katika maonyesho ya nguvu ya mshikamano na watu wa Palestina na kutaka kukomeshwa haraka mauaji ya halaiki yanayofanywa na utawala wa kibaguzi wa Israel huko Gaza.
Vile vile idadi kubwa ya wananchi wa Denmark wameonyesha mshikamano wao na wananchi wa Palestina kwa kufanya maandamano katika mitaa ya "Copenhagen" kwa ajili ya kuunga mkono Palestina hususan watu wa Ukanda wa Gaza.
Waungaji mkono wa wananchi wa Palestina katika maeneo mbalimbali ya dunia wamekuwa wakifanya maandamano katika miezi ya hivi karibuni kulaani vikali jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza.

Hali kadhalika baada ya takriban miezi 9 ya uvamizi wa Israel usio na tija katika Ukanda wa Gaza, utawala huo haujafanikiwa lolote katika medani ya vita zaidi ya kutekeleza mauaji ya umati, uharibifu, jinai za kivita, ukiukaji wa sheria za kimataifa, ulipuaji wa mashirika ya misaada ya kibinadamu na kusababisha njaa kali kwa Wapalestina katika ukanda huo uliozingirwa.