Sadiq Khan: Usalama umeimarishwa katika misikiti ya London
Meya wa jiji la London ametangaza kuongezwa hatua za usalama katika mji huo ikiwa ni pamoja na mafunzo katika misikiti katika mji mkuu huo wa Uingereza.
Meya wa London Sadiq Khan ameapa kuungana dhidi ya ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Uislamu na chuki dhidi ya Wayahudi, kufuatia vuruguhasia na ghasia za hivi karibuni kote nchini Uingereza ambazo zimewatia hofu watu wengi wa jamii za walio wachache nchini humo.
Polisi wa Uingereza wametangaza kuwa zaidi ya watu 700 wametiwa mbaroni wakati wa machafuko na matukio ya vurugu za mrengo wa kulia wenye misimamo mikali nchini humo, na inatarajiwa kwamba idadi ya wanaokamatwa itaongezeka kutokana na kushadidi ghasia hizo.
Ghasia kubwa zilianza katika aghalabu ya miji ya Uingereza mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, baada ya barobaro mmoja mwenye umri wa miaka 17 kushambulia hafla iliyokuwa ikifanyika katika shule moja ya watoto katika mji wa Southport.
Watoto watatu waliuawa katika hujuma hiyo. Watoto wengine kadhaa na watu wazima wawili waliokuwa wamejeuhiwa vibaya, walipelekwa hospitali kufuatia shambulio hilo la kisu. Mara tu baada ya tukio hilo, habari za uongo zilichapishwa katika vyombo vya habari vya Uingereza kwamba barobaro huyo alikuwa mhajiri Mwislamu. Wafuasi wenye misimamo ya kufurutu ada wa mrengo wa kulia walitumia vibaya taarifa hiyo ya uongo kama kisingizio cha kuanza kuwashambulia Waislamu, vituo na maneo yao ya ibada.