China: Tunapinga ukiukwaji wa mamlaka ya kitaifa ya mataifa
(last modified Mon, 28 Oct 2024 11:15:43 GMT )
Oct 28, 2024 11:15 UTC
  • China: Tunapinga ukiukwaji wa mamlaka ya kitaifa ya mataifa

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China amesema kuwa, Beijing inapinga vikali hatua ya kukiukwa mamlaka ya kitaifa ya mataifa mengine.

Lin Jian amesema hayo akijibu hatua ya hivi karibuni ya kichokozi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran na kusisitiza kwamba, China inapinga hatua yoyote ya kukiuka mamlaka ya kitaifa na usalama wa nchi nyingine na kutumia nguvu na mabavu mtawalia.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China ameongeza kuwa, hali ya sasa katika Asia Magharibi ni ya wasiwasi sana na wahusika wanapaswa kujiepusha na kuongeza hatari za usalama katika eneo hilo.

Kadhalika, vile vile amesema, baadhi ya matukio kwa mara nyingine tena yameonyesha udharura na ulazima wa kusitishwa mapigano na kuhitimisha vita. Jumuiya ya Kimataifa, hasa madola yenye ushawishi, yanapaswa kuwa na jukumu la kujenga na kuchukua hatua muhimu katika kupunguza mivutano ya kikanda.

Radiamali hiyo ya China inafuatia hatua ya utawala wa Kizayuni jjuzi Jumamosi alfajiri  ya kushambulia baadhi ya kambi za kijeshi katika mikoa ya Tehran, Khuzistan na Ilam ambapo mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran ulifanikiwa kuzima hujuma hiyo na kukabiliana na hatua za kichokozi za utawala wa Kizayuni.