UNICEF: Zaidi ya watoto 200 wameuawa Lebanon katika mashambulizi ya Israel
(last modified Wed, 20 Nov 2024 08:08:47 GMT )
Nov 20, 2024 08:08 UTC
  • UNICEF: Zaidi ya watoto 200 wameuawa Lebanon katika mashambulizi ya Israel

Huku dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watoto, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema zaidi ya watoto 200 wameuawa nchini Lebanon tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo miezi miwili iliyopita.

UNICEF imewaambia waandishi wa habari kwamba, wastani wa watoto watatu wameuawa kila siku nchini Lebanon, huku Israel ikiendeleza mashambulizi kote nchini humo.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeonya kwamba, kama ilivyo huko Gaza, "wale walio na ushawishi" wameshindwa kuchukua hatua ya maana huko Lebanon licha ya hali mbaya ya watoto.

Msemaji wa UNICEF, James Elder, amewaambia waandishi wa habari kwamba: "Licha ya watoto zaidi ya 200 kuuawa nchini Lebanon (kwenye mashambulizi ya Israel) katika kipindi cha chini ya miezi miwili, hali ya kutatanisha imeibuka; Mauaji yao yamepuuzwa na wale ambao wanaweza kukomesha ukatili huo." 

James Elder ameongeza kuwa: "Kwa watoto wa Lebanon, imekuwa hali ya kawaida na ya kutisha."

Msemaji wa UNICEF ameorodhesha angalau mashambulizi sita kote Lebanon ambapo watoto wameuawa katika mashambulizi ya Israel, mara nyingi pamoja na familia zao, katika muda wa siku 10 zilizopita.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amebainisha "kufanana kwa kutisha" kati ya kile kinachotokea kwa watoto huko Lebanon na wale wa Gaza, ambayo imekumbwa na mashambulizi ya anga ya Israel kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Israel imeua karibu watoto 17,400 huko Gaza.

Leo na katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watoto, jumuiya na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yametoa wito wa kukomeshwa mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel huko Gaza na Lebanon ambayo wahanga wake wengi ni watoto wadogo.