Jaji: Hukumu dhidi ya Trump kutolewa kabla ya kuapishwa kwake
(last modified Sun, 05 Jan 2025 03:35:04 GMT )
Jan 05, 2025 03:35 UTC
  • Jaji: Hukumu dhidi ya Trump kutolewa kabla ya kuapishwa kwake

Jaji wa New York ametangaza kuwa, hukumu dhidi ya Donald Trump Rais mteule wa Marekani itatolewa tarehe 10 ya mwezi huu wa Januari katika kesi yake ya fedha mjini New York siku chache kabla ya kuapishwa kuwa rais.

Jaji wa New York Juan Merchan aliashiria kuwa hatamhukumu Trump kifungo cha jela, mashtaka au faini, lakini badala yake "atamuachilia bila masharti", na akaandika kwamba rais mteule anaweza kufika mahakamani binafsi au kwa njia ya mtandao kwa ajili ya kusikilizwa.

Trump alijaribu kutumia ushindi wake wa urais ili kesi dhidi yake ifutwe.

Rais huyo mteule amechapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akitupilia mbali amri ya jaji huyo  na kuitaja hatua hiyo kama "shambulio la kisiasa lisilo halali" na kuiita kesi hiyo kuwa "hakuna chochote isipokuwa ni wizi wa kura".

Trump alipatikana na hatia mwezi Mei kwa makosa 34 ya kughushi rekodi za biashara zinazohusiana na malipo ya $130,000 (£105,000) kwa nyota wa filamu za watu wazima Stormy Daniels.

Mashtaka yanayohusiana na majaribio ya kuficha malipo kwa mwanasheria wake wa zamani, Michael Cohen, ambaye katika siku za mwisho za kampeni za uchaguzi wa 2016 alimlipa pesa nyota huyo wa filamu za watu wazima ili kukaa kimya kuhusiana na madai ya kukutana na Trump.