Kwa nini Trump hastahamili kuwepo kwa wahamiaji Waislamu huko Marekani?
-
Donald Trump
Moja ya amri tisa za Donald Trump katika siku ya kwanza ya uongozi wake ni kupitiwa upya sheria ya kurejesha marufuku ya Waislamu kuingia Marekani, suala ambalo iwapo litaidhinishwa na kutekelezwa, litakuwa na madhara makubwa kwa wahamiaji Waislamu nchini Marekani na hata waombaji visa Waislamu.
Baada ya kutolewa amri hiyo mpya ya utendaji ya Donald Trump, watetezi wa haki za kiraia nchini Marekani wameitambua kuwa ina maana pana zaidi kuliko ile iliyotolewa mwaka wa 2017 wakati wa utawala wa kwanza wa Trump, na kuonya dhidi ya utekelezaji wake. Watetezi wa haki za kiraia wa Marekani wametangaza kwamba amri hiyo itafungua njia ya kuwalenga raia wa kigeni wanaoishi kisheria nchini Marekani, pamoja na kuhalalisha ukandamizaji wa wanafunzi wa kimataifa wanaotetea haki za Wapalestina.

Sheria ya kupiga marufuku Waislamu kuingia Marekani, hasa kutoka nchi kadhaa zenye Waislamu wengi, zikiwemo Syria, Libya, Yemen, Sudan na Iran, ilitiwa saini na kutekelezwa wakati wa muhula wa kwanza wa urais wa Trump 2017. Sheria hiyo ilikabiliwa na upinzani, maandamano na changamoto za kisheria wakati wa utekelezaji wake, kwa kwa msingi huo ilifutwa wakati wa utawala wa Joe Biden. Sasa, Trump ametoa wito wa kupigwa marufuku wahajiri Waislamu kuingia nchini Marekani na ameahidi kuitekeleza sheria hiyo kwa kiwango kikubwa zaidi.
Joe Burton, afisa wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje na afisa wa Idara ya Visa ya Marekani, amesema agizo hilo jipya linaweza kuipa serikali mamlaka mapana yasiyo na mpaka ya kuwanyima visa wanafunzi, wafanyakazi na washiriki katika vikao na shughuli za kubadilishana maarifa.
Uamuzi huu wa serikali ya Trump unakuja wakati Marekani imekuwa ikidai kuwa ni nchi huru inayoheshimu uhuru wa kiraia, kijamii na wa mtu binafsi, kaulimbiu ambazo zimekuwa zikihojiwa zaidi na kutajwa kuwa ni porojo na bwabwaja tupu za Donald Trump.
Inaonekana kuwa, kustawi kwa harakati mpya za kijamii zinazopigania uhuru na kutetea thamani za kimataifa nchini Marekani hususan katika miaka ya hivi karibuni ambazo zimesababisha makumi ya maandamano ya kupinga jinai za Israel katika vita vya Gaza, kumewakasirisha viongozi wa Washington.
Katika kipindi cha miezi michache iliyopita, wakati jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza zilipoongezeka, maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu na raia wa Marekani walifanya maandamano wakiilaani Israel na washirika wake. Maandamano hayo yalikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa polisi kiasi kwamba wanafunzi wengi walikamatwa au kufukuzwa kutoka vyuo vikuu vingi vya Marekani. Siku chache ziliopita, gazeti la Kiebrania, Yedioth Ahronoth, liliandika kuhusiana na hilo kwamba: Baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump ameahidi kuzipiga faini taasisi za kitaaluma ambazo, eti hazitakabiliana na alichodai ni "wendawazimu na watetezi wa Palestina."

Inaonekana kuwa Trump anakusudia kurasimisha hatua hizo katika kalibu ya kuweka sheria inayowapiga marufuku wahajiri Waislamu kuingia Marekani.
Rais mpya wa Marekani sio tu kwamba hana dhamira ya dhati ya kutekeleza kaulimbiu za kutetea uhuru na za kibinadamu, bali pia anataka kukanyaga nara zote na kuandaa njia ya kuwatimua wale wote wanaowaunga mkono na kuwatetea watu wa Palestina kwa njia yoyote ile.