Hungary: Baadhi ya nchi za Ulaya zinakwamisha kumalizika vita huko Ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary amesema kuwa "Waliberali wa Ulaya wanaounga mkono vita" wanakwamisha kufanyika mazungumzo ya amani kati ya Marekani na Russia ili kuhitimisha vita huko Ukraine.
Peter Szijjarto ameeleza kuwa: Nchi za Ulaya hazitakubali kutoa mabilioni mengine ya yuro (Euro) kwa ajili ya kununulia silaha za Ukraine. Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary amebainisha haya katika kukaribia kufanyika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya huko Brussels Ubelgiji.
Nchi za Ulaya zinapanga kuidhinisha kitita kingine cha msaada wa kijeshi kwa Ukraine, wenye thamani ya karibu yuro bilioni 6. Zinadai kuwa lengo la msaada huu wa fedha ni kuimarisha msimamo wa kimkakati wa Kiev kabla ya kufanyika mazungumzo ya amani chini ya uongozi wa Marekani na Russia.
Szijjarto ameeleza hivi na ninamnukuu:" Kwa miaka mitatu sasa tumekuwa tukipinga mashinikizo dhidi yetu; ambapo hatujakubali kutumbukizwa katika sera hii ya vita, na tutaendelea kukabiliana nayo."