Baadhi ya Waislamu waanza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani
Baadhi ya mataifa ya Kiarabu na Kiislamu Jumamosi ya leo yameanza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Baadhi ya mataifa ya Kiarabu na Kiislamu ikiwemo Saudi Arabia, Misri, Qatar, Imarati, Bahrain, Oman, Lebanon, Morocco, Palestina, Tunisia, Mauritania, Indonesia na Malaysia yametangaza kuwa, leo ni tarehe Mosi Ramadhani. Nchini Uganda pia Baraza Kuu la Waislamu nchini humo limetangaza kuwa, leo ni tarehe Mosi Ramadhani ambapo sambamba na kutoa taarifa hiyo limewatakia Waislamu wa nchi hiyo na wa dunia nzima funga njema ya Ramadhani.
Wakati huo huo, mataifa mengine ya Kiislamu na Kiarabu ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yanatarajiwa kuanza funga ya Ramadhani Jumapili ya kesho.
Ayatullah Sayyid Ali Sistani, Kiongozi wa juu wa kidini na Marjaa-Taqlidi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq na Marajii wengine wa Kishia wametangaza kuwa, Jumapili ya kesho itakuwa siku ya kwanza ya mwezi wa Ramadhani.
Nchini Tanzania Sheikh Abubakry Zubeir bin Ali Mufti na Sheikh Mkuu wa nchi hiyo ametangaza kuwa jana Ijumaa mwezi haukuandama hivyo Waislamu wa nchi hiyo wataanza funga ya Ramadhani kesho Jumapili.
Aidha kwa mujibu taarifa iliyotolewa na kamati ya kuangalia mwezi mwandamo ya Waislamu wa Madhehebu ya Shia nchini Tanzania jana mwezi haukuandama hivyo leo ni tarehe 30 Shaaban na kesho itakuwa siku ya kwanza ya mwezi wa Ramadhani. Kwa upande wa Kenya Waislamu wa nchi hiyo wamegawanyika ambapo kuna wanaoanza funga ya Ramadhani leo huku Kadhi Mkuu wa nchi hiyo akitangaza kuwa, mwezi haukuandama jana, hivyo Waislamuu wataanza funga ya Ramadhani Jumapili ya kesho.