Kuanza tena Marekani kuipa Ukraine silaha, Putin atoa masharti
(last modified Sat, 15 Mar 2025 02:23:29 GMT )
Mar 15, 2025 02:23 UTC
  • Kuanza tena Marekani kuipa Ukraine silaha, Putin atoa masharti

Sambamba na kujaribu kuonesha kuwa msimamo wa Marekani umebadilika kuhusu Russia, rais wa Marekani, Donald Trump hivi sasa anapanga kupeleka shehena mpya ya silaha kwa Ukraine ili kuendeleza vita na Russia ikiwa ni kuonesha siasa zilezile za kila siku za nyuso mbili za Marekani.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa Marekani inapanga kuipa Ukraine shehena mpya ya silaha za masafa marefu kama mabomu madogo yanayorushwa kutokea ardhini yaitwayo (GLSDB). Silaha hizi, zilizoboreshwa ni maalumu kwa ajili ya kukabiliana na vita vya kielektroniki vya Russia na zinaweza kuisaidia Ukraine kulenga shabaha kwa usahihi zaidi.

Hatua hiyo imekuja huku taarifa zikisema kuwa, akiba ya Ukraine ya Mfumo wa Makombora ya Marekani (ATACMS) ambazo ni silaha nyingine ya masafa marefu ilizopewa Ukraine, imepungua.

Duru mbili zenye welewa wa kutosha kuhusu suala hilo ambazo hazikutaka majina yao kutangazwa kwenye vyombo vya habari zimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba mabomu hayo mapya yametengenezwa maalumu kwa ajili ya kukabiliana na vita vya kielektroniki vya Russia ambavyo hada sasa vimeiweka Ukraine kwenye wakati mgumu kutokana na kuvuruga mara kwa mara mifumo yake ya kivita. 

Kyiv, mji mkuu wa Ukraine ulivyosambaratishwa vibaya na vita

 

Marekani imeamua kuisheheneza Ukraine silaha mpya katika hali ambayo huyo huyo Donald Trump ambaye hapa anaonekana wazi akichochea moto wa vita, alidai juzi Alkhamisi kuwa anakaribisha mazungumzo ya amani kati ya Russia na Ukraine. Alidai kuwa, yeye na washauri wake wamejadiliana masuala mbalimbali kuhusu namna ya kumaliza vita vya Ukraine.

Trump amedai kuwa, mazungumzo hayo yanaweza kuleta mabadiliko katika mpaka wa kimataifa kati ya nchi hizo mbili, lakini hakutoa maelezo zaidi. "Hili ni suala gumu," alisema.

Wakati huo huo, duru za kuaminika zimeiambia televisheni ya CBS ya Marekani kwamba sambamba na uamuzi wake wa kuipa Ukraine silaha mpya, utawala wa Trump unapanga pia kuweka vikwazo zaidi dhidi ya sekta ya mafuta, gesi na benki ya Russia. Duru hizo zimesema, hatua hiyo inaweza kutajwa kuwa ni vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Russia.

Kwa kuzingatia yote hayo, Rais Vladimir Putin wa Russia amesema, anakubaliana na wazo la kusitisha mapigano kwa siku 30 na Ukraine lakini kwa sharti kwamba kuchukuliwe hatua za kuonesha nia njema na usimamishaji vita huo upelekee kupatikana amani ya kudumu na kuzingatiwa daghadagha zote za Moscow. 

Rais Putin alisema hayo Alhamisi jioni ikiwa ni majibu yake ya kwanza rasmi kwa pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano kwa muda wa siku 30 nchini Ukraine.

Katika sehemu moja ya matamshi yake, Putin alisema: "Tunakubali kusitisha mapigano kwa siku 30 kwa sharti kwamba hatua hiyo ilete amani ya kudumu na kuondoa mizizi ya mgogoro."

Marais wa Russia na Marekani

 

Wakati huo huo lakini Rais wa Russia alitoa onyo kali kwa wanajeshi wa Ukraine walioko Kursk, akisema: "Mna machaguo mawili tu; imma mujisalimishe au mtauawa."

Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusu masharti yake, Rais Putin alisema: "Ikiwa tutasimamisha vita kwa siku 30, je, hiyo itakuwa na maana kwamba vikosi vyote vya Ukraine vitaondoka Kursk? Hatuwezi kuwaachilia kubakia baada ya kuwa wamefanya uhalifu mwingi."

Rais wa Russia amekwenda mbali zaidi na kusema: "Naweza kumpigia simu Trump kuzungumza naye kuhusu usitishaji vita. Ikiwa Marekani na Russia zitafikia makubaliano kuhusu ushirikiano wa nishati, bomba la gesi nalo linaweza kupatikana kwa ajili ya nchi za Umoja wa Ulaya."

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kama si uungaji mkono wa madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani kwa serikali kibaraka ya Kyiv, vita vya Ukraine vingelikuwa vimemalizika muda mrefu nyuma. Hivi sasa pia rais wa Marekani anaonekana kuendelea na siasa zilezile za kutumia vikwazo na mashinikizo kama njia ya kufikia malengo yake. Hatua ya Trump ya kuisheheneza Ukraine silaha mpya za kukabiliana na Russia na wakati huo huo kudai kuwa anataka amani na vita vikomeshwe huko Ukraine, ni muendelezo wa siasa hizo hizo za kiistikbari za Marekani.