EU na Uingereza kuongeza mashinikizo dhidi ya Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i124062-eu_na_uingereza_kuongeza_mashinikizo_dhidi_ya_russia
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imesema kuwa, kutafanyika kikao baina yao na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya ili kuzidisha mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya Russia.
(last modified 2025-03-18T07:58:22+00:00 )
Mar 18, 2025 07:58 UTC
  • EU na Uingereza kuongeza mashinikizo dhidi ya Russia

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imesema kuwa, kutafanyika kikao baina yao na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya ili kuzidisha mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya Russia.

Gazeti la Die Welt limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Umoja wa Ulaya na Uingereza zinataka kushadidisha mashinikizo dhidi ya Russia na kuimarisha mipango yao ya ulinzi dhidi ya Moscow.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imesema katika taarifa yake kwamba: Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaia Kallas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lamy na Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, John Healy walikuwa wakutane leo Jumanne.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mazungumzo hayo pia yatalenga kuimarisha hatua za pande hizo za kukabiliana na vitisho vya pamoja kama vile mashambulizi ya mtandaoni, kuingiliwa chaguzi na kuenea taarifa zisizo sahihi.

Aidha ilikuwa imepangwa kwamba leo Jumanne, Kansela wa Ujerumani Olaf Schulz awe mwenyeji wa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mjini Berlin.

Hatua hizo za nchi za Ulaya dhidi ya Russia zimekuja katika hali ambayo, siku chache zilizopita na sambamba na kujaribu kuonesha kuwa msimamo wa Marekani umebadilika kuhusu Russia, rais wa Marekani, Donald Trump aliamua kupeleka shehena mpya ya silaha kwa Ukraine ili kuendeleza vita na Russia. Hatua hiyo ya Trump ilihesabiwa kuwa ni muendelezo wa siasa zilezile za kila siku za nyuso mbili za Marekani.