Ubelgiji yajibu: Wanadiplomasia wa Rwanda hawatakiwi nchini mwetu
Ubelgiji imejibu hatua ya Rwanda ya kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na nchi hiyo ya Ulaya na kusema kuwa, wanadiplomasia wa Rwanda wanapaswa kuondoka nchini Ubelgiji. Hatua hiyo imekuja huku uhusiano baina ya nchi hizo mbili ukizidi kuharibika kutokana na mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Maxime Prevot amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Ubelgiji imesikitishwa na uamuzi wa Rwanda wa kukata uhusiano wa kidiplomasia na Ubelgiji na kutangaza kuwa wanadiplomasia wa Ubelgiji hawatakiwi kuweko Rwanda. Sisi pia tunasema, wanadiplomasia wa Rwanda hawatakiwi tena nchini Ubelgiji."
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji amesema: "Rwanda wanapendelea kutoshiriki kwenye mazungumzo."
Hatua ya Rwanda ya kukata uhusiano wa kidiplomasia na Ubelgiji imekuja siku moja baada ya Rais Paul Kagame kuishutumu nchi hiyo ya Ulaya kuwa inatetea kuwekewa Kigali vikwazo vya kimataifa kutokana na mgogoro wa mashariki mwa DRC.
Kwa mujibu wa televisheni ya Al Jazeera ya Qatar, kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda lilifanya mashambulizi makubwa katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa DRC mapema mwaka huu na kuteka miji miwili mikubwa kwa kasi sana.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, Rwanda ndiyo inayolimiliki na kulidhibiti kundi hilo na kuna takriban wanajeshi 4,000 wa Rwanda ndani ya ardhi ya DRC. Kigali imekuwa ikikanusha kuhusika na mzozo huo na kusema inakabiliwa na tishio kutoka kwa wapiganaji wa kabila la Wahutu wa nchini DRC.
Serikali ya DRC imesema takriban watu 7,000 wameshauawa kwenye mgogoro huo na imetaka kuchukuliwe hatua za haraka za kimataifa kukomesha maafa ya raia wa mashariki mwa nchi hiyo.
Mvutano wa kidiplomasia uliongezeka jana Jumatatu baina ya Rwanda na Ubelgiji huku serikali ya DRC na waasi wa M23 wakitangaza kupeleka wajumbe wao kwenye mazungumzo ya amani, ambayo yalipangwa kufanyika leo Jumanne nchini Angola. Mazungumzo hayo hayakufanyika tena baada ya waasi wa M23 kutangaza kujitoa.