Maandamano yarindima Meya wa Istanbul, hasimu wa Rais wa Uturuki alipokamatwa
Maelfu ya wananchi wa Uturuki wamemiminika barabarani kulalamikiwa kutiwa mbaroni Meya wa Istanbul, Ekrem Imamoglu, mpinzani mkuu wa kisiasa wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambaye amekamatwa kwa tuhuma za rushwa na ugaidi; siku chache kabla ya kuteuliwa kuwa mgombea wa urais.
Shirika la serikali la Anadolu limesema Imamoglu alikamatwa jana Jumatano, na kwamba Waendesha Mashtaka pia wametoa waranti dhidi watu wengine 100, wakiwemo wanasiasa wa Uturuki, waandishi wa habari na wafanyabiashara.
Anadolu imewanukuu Waendesha Mashtaka wakisema kuwa, Imamoglu - kutoka chama cha kisekula cha Republican People's Party (CHP) - anatuhumiwa kuwa "mshukiwa mkuu wa shirika la uhalifu."
Ofisi ya Gavana wa Istanbul imeweka vizuizi katika jiji hilo kwa kufunga barabara kadhaa na kupiga marufuku maandamano ya siku nne, katika juhudi zinazoonekana ni za kukomesha "vitendo vinavyowezekana kuwa vya uchochezi" kufuatia kukamatwa kwa mwanasiasa huyo.

Kukamatwa huko kunakuja wakati CHP ilitazamiwa kufanya uchaguzi wa mchujo mnamo Machi 23, ambapo Imamoglu alitarajiwa kuchaguliwa kama mgombeaji wake wa urais, na kura inayofuata ya urais ikitarajiwa 2028 wakati uchaguzi wa mapema unawezekana.
"Irada ya watu haiwezi kuzimwa," Imamoglu ameandika kwenye mtandao wa kijamii. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 53 katika video iliyosambaa mtandaoni, amewataka Waturuki na watu wote wanaotetea demokrasia na haki duniani kote "kusimama kidete kwa ajili ya watu wa Uturuki." Amesema, "Ninasimama kidete katika kupigania haki za kimsingi na uhuru."