Serikali Uturuki yawaonya waandamanaji, wapinzani waapa kuyaendeleza
Serikali ya Uturuki imeonya dhidi ya wito iliosema ni "haramu" wa kambi ya upinzani kufanya maandamano mitaani ili kupinga kukamatwa Meya wa Istanbul, Ekrem Imamoglu, kufuatia maandamano ya maelfu ya watu kote nchini katika muda wa siku mbili zilizopita.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Ali Yerlikaya amesema watu 53 wamekamatwa, na maafisa 16 wa polisi wamejeruhiwa katika maandamano hayo yaliyoanzia kwenye vyuo vikuu, makao makuu ya Manispaa ya Istanbul na maeneo mengine siku ya Alkhamisi, huku kukishuhudiwa mapigano na makabiliano makali kati ya waandamanaji na askari usalama.
Maandamano hayo yameibuka katika miji yote ya Uturuki baada ya mpinzani wa Rais Recep Tayyip Erdogan, Ekrem Imamoglu kukamatwa na vyombo vya dola kwa madai ya kuhusika na ufisadi.
Meya wa Istanbul, Ekrem Imamoglu, alizuiliwa siku ya Jumatano iliyopita. Alitiwa nguvuni katika uvamizi uliofanyika alfajiri katika nyumba yake akihusishwa na ufisadi, hongo na kuwa na uhusiano wa ugaidi.
Wanasiasa wengi, wafanyabiashara na maafisa wa manispaa wanaohusishwa na meya huyo pia wamekamatwa.
Kukamatwa kwa meya huyo kunatazamwa kama jaribio la kisiasa la kumuondoa mpinzani mkuu wa Erdogan katika uchaguzi ujao wa urais nchini Uturuki.
Imamoglu, ambaye anatoka Chama cha Republican People’s Party (CHP), alisema muda mfupi kabla ya kukamatwa kwamba "irada ya watu haiwezi kunyamazishwa."
Kukamatwa kwa Ekrem Imamoglu, 54, ambaye amehudumu kwa mihula miwili kama Meya wa Istanbul, kumekuja siku chache kabla ya Chama cha Republican People's Party (CHP) kumteua kuwa mwenyekiti wake katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Jumapili wiki hii.
Uchunguzi wa maoni uliofanyika Jumatano iliyopita ulionyesha kuwa Ekrem Imamoglu anamtimulia kivumbi Rais Recep Tayyip Erdoğan. Uchaguzi ujao wa urais umepangwa kufanyika 2028.