Maelfu waandamana mjini London katika Siku ya Kimataifa Quds kutetea Palestina
Maandamano ya Siku ya Quds ya Kimataifa mwaka huu yamefanyika mapema jijini London Jumapili, Machi 23, na kuvutia maelfu ya washiriki kutoka nyanja mbalimbali ili kutetea haki za Wapalestina na kulaani jinai za utawala haramu wa Israel
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds ya London yamelanga kuhamasisha ufahamu kuhusu janga la kibinadamu huko Palestina hasa katika Ukanda wa Gaza. Aidha maandamano hayo yametumika kama jukwaa la kupaza sauti za wanaopinga dhuluma na ubaguzi dhidi ya Wapalestina.
Tukio hilo limeakisi harakati inayokua duniani ambayo inawaunganisha watu kutoka dini na mataifa mbalimbali katika mshikamano na watu wa Palestina.
Washiriki wa tukio hilo wameonyesha hasira zao, wakisema kwamba "utawala wa Kizayuni wa Israel umeua zaidi ya Wapalestina 50,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha mwaka moja na nusu uliopita.
Washiriki wamekemea nchi za Ulaya na Marekani kwa kushirikiana na utawala katili wa Israel katika mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.
Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu London, ambayo imekuwa ikiandaa maandamano ya Siku ya Quds nchini Uingereza kwa zaidi ya miaka 40, imefanikiwa kuwaleta pamoja wafuasi wa dini zote ili kusimama dhidi ya jinai za Israel dhidi ya Wapalestina.
Tukio hilo lilimalizika nje ya makao makuu ya Shirika la utangazaji la BBC, ambapo wazungumzaji walikemea msaada wa silaha wa serikali ya Uingereza kwa Israel.
Licha ya kuongezeka ukandamizaji nchini Uingereza maandamano hayo ya Siku ya Kimataifa ya Quds yanasalia kuwa jukwaa la mjumuiko wa familia na wanaharakati wanaotetea haki na uhuru kwa Palestina.
Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu London yamefanyika siku ya Jumapili, ambayo ni siku ya mapumziko nchini badala ya Ijumaa ya mwisho ya Ramadhani ambayo ni siku ya kazi nchini humo.