Wimbi jipya la maandamano dhidi ya Uzayuni barani Ulaya
Maandamano makubwa yamefanyika huko Paris mji mkuu wa Ufaransa na katika miji mingine ya Ulaya kupinga duru mpya ya mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Maamandamano hayo yanadhihirisha ghadhabu na upinzani wa walimwengu kwa hatua za Israel na ni radiamali ya harakati ya kimataifa kwa ajili ya kuwatetea wananchi wa Palestina na kulaani jinai za Wazayuni. Wimbi la hasira na kuchukizwa walimwengu na mauaji ya kimbari na mshambulizi mapya ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza limeenea kuanzia Vienna hadi Stockholm, kuanzia Auckland hadi Berlin.
Washiriki katika maandamano hayo barani Ulaya wanasisitiza kuwa kile kinachojiri hivi sasa huko Gaza ni maafa ya binadamu na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa kwa ushirikiano na katika kalibu ya kimya cha serikali za Magharibi. Huko Paris, waandamanaji wamepiga nara na shaari kama "Palestina inapasa kukombolewa" na "Sitisha mauaji dhidi ya Gaza" na kutaka kusimamishwa haraka iwezekanavyo himaya na misaada ya kijeshi na kisiasa kwa Israel. Polisi wa Ufaransa wameamiliana kwa mabavu na waandamanaji na kwa mara nyingine kudhihirisha misimamo ya undumakuwili ya serikali za Magharibi mkabala wa uhuru wa kujieleza na haki za binadamu. Huko Ujerumani na Uingereza pia maelfu ya watu wameandamana kupinga na kulaani sera za serikali za nchi hizo za kuiunga mkono Israel. Nukta ya kuzingatia hapa ni ushiriki mkubwa wa vijana, wanaharakati wa mrengo wa kushoto na hata baadhi ya makundi ya Kiyahudi yanayopinga Uzayuni katika maandamano hayo, jambo linaonyesha kuwa mijadala mikuu katika vyombo vya habari vya Magharibi ambayo inataja ukosoaji wowote wa Israel kuwa ni “chuki dhidi ya Wayahudi” haiwezi tena kudhibiti maoni ya umma kwa urahisi.
Huko Paris maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi yaligeuka na kuwa maandamano dhidi ya Uzayuni na kulaaniwa kukiukwa makubabaliano ya kusimamisha vita na kuanza duru mpya ya mashambulizi ya jeshi la utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza. Waandamanaji huko Paris wametaka wananchi wa Palestina waungwe mkono na watendewe haki huko Gaza na katika Ukingo wa magharibi na viongozi wa Kizayuni wahukumiwe katika mahakama za kimataifa.
"Peter Leary" kutoka Harakati ya Mshikamano wa Palestina nchini Uingereza amesema: "Kwa muda wa miezi 17, tumesimama na kudhihirisha mshikamano na wananchi wa Palestina katika nyakati za giza kabisa za historia yao, wakikabiliwa na mauaji ya kutisha yaliyofanywa na Israel." "Kusalia kimya Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri wetu Mkuu Keir Starmer kumepelekea kuuliwa mamia ya watu katika siku kadhaa zilizopita na kutolewa onyo za kuendelea mauaji hayo. Hata viongozi wa Uingereza hawawezi kuakisi katika vyombo vya habari matamshi yanayokosoa jinai za Wazayuni."
"David Lammy Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza jana Jumatatu alisema katika taarifa kuwa Israel inakiuka sheria za kimataifa. "Mara baada ya kutoa matamshi haya, Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Uingereza alibatilisha kauli yake kufuatia mashinikizo ya Starmer. Kukiri kwamba Israel inatenda jinai ina maana ya kukiri kuhusu kushiriki Uingereza katika jinai hizo. Lindsey German mwanachama wa Muungano Unaopinga Vita wa nchini Uingereza wa "Stop the War Coalition" amesema: "Je, tuone jinai ngapi zaidi za kivita huko Gaza kabla ya serikali kutambua kuwa ni mauaji ya kimbari? Starmer sasa ndiye mfadhili mkubwa zaidi wa silaha barani Ulaya, akitumia pesa nyingi kuifadhili Israel. Mwanachama huyu wa Muungano Unaopinga Vita ameongeza kuwa: "Sisi hapa kwetu Uingereza tumekuwa tukipigania uhuru wa kusema vizazi kwa vizazi. Ubalozi wa Israel ndio ubalozi pekee ambao hauwezi kuandamana mbele yake moja kwa moja."
Maandamano ya kupinga jinai za Wazayuni yamegeuka kuwa harakati kubwa katika nchi za Magharibi tangu kuanza mashambulizi ya kikatili na mauaji ya kimbari ya Wazayuni katika Ukanda wa Gaza mwezi Oktoba 2023. Vitisho vya serikali za Magharibi dhidi ya washiriki wa "Harakati ya Kupinga Uzayuni" havijapunguza maandamano na mijumuiko dhidi ya Israel katika nchi hizo. Hata baadhi ya Wayahudi wanaoishi katika nchi za Magharibi pia wamejiunga na harakati hiyo. Taasisi kwa jina la "Umoja wa Wayahudi wa Ufaransa kwa ajili ya Amani" imeendesha semina huko Paris kwa lengo la kukabiliana na hatari ya hujuma za uvamizi za Israel katika eneo na kusisitiza juu ya ulazima wa kuwawajibisha viongozi wa utawala ghasibu kwa mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.