China yasema inaunga mkono Misri dhidi ya 'ubabe’ wa Trump
(last modified Sat, 10 May 2025 04:27:24 GMT )
May 10, 2025 04:27 UTC
  • China yasema inaunga mkono Misri dhidi ya 'ubabe’ wa Trump

China imeonyesha uungaji mkono kwa mamlaka na maslahi ya Misri ikiwemo juu ya Mfereji wa Suez kufuatia matamshi ya ubabe ya rais wa Marekani.

Msimamo wa China umekuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kudai kupitia Truth Social, jukwaa lake la mitandao ya kijamii, kwamba Marekani inapaswa kupatiwa ruhusa ya meli za kibiashara na za kijeshi za Marekani kupita bila malipo katika Mifereji ya Panama na Suez, ombi ambalo Misri imepinga vikali.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian, katika mkutano na waandishi wa habari amesema: “China inaunga mkono kwa dhati serikali na watu wa Misri katika kulinda mamlaka yao na haki na maslahi yao halali, na inapinga maneno au vitendo vyovyote vya ubabe."

Mwezi uliopita, Trump alidai kwenye Truth Social kwamba bila Marekani, Mifereji ya Panama na Suez isingekuwepo, na kwa hivyo meli za kibiashara na za kijeshi za Marekani zinapaswa kupewa ruhusa ya kupita bila kulipa ada yoyote, akiongeza kuwa amemwagiza Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio kufuatilia suala hilo.

Gazeti la The Wall Street Journal liliripoti kuwa Trump alimwambia mwenzake wa Misri, Abdel Fattah Al-Sisi, kwamba alikuwa akitafuta kuhakikisha meli za Marekani zinapita bure kupitia Mfereji wa Suez.

Gazeti hilo lilinukuu vyanzo vikisema kuwa Trump alionyesha nia ya kupata msaada kutoka Cairo katika operesheni dhidi ya harakati ya Ansarullah ya Yemen, hususan msaada wa kijeshi, kubadilishana taarifa za kijasusi, au ufadhili. Hata hivyo, Al-Sisi alikataa ombi hilo, akibainisha kuwa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza ndilo suluhisho bora zaidi la kuzuia Ansarullah kutekeleza operesheni za kijeshi.