Marekani yaendelea kuwakandamiza wanafunzi wanaotetea Palestina
-
Rumeysa Ozturk
Jaji mmoja nchini Marekani amemuachilia kwa dhamana mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tufts ambaye ni mtetezi wa Palestina, Rumeysa Ozturk, kutoka kizuizi cha uhamiaji cha Louisiana, huku serikali ya Donald Trump ikiendelea kuwakandamiza wanafunzi wa vyuo vikuu wanaoandamana kuunga mkono Palestina na kulaani jinai za Israel.
Ozturk, mwanafunzi wa shahada ya uzamivu kutoka Uturuki, alikuwa akishikiliwa na mamlaka za uhamiaji za Marekani tangu Machi 25, alipokamatwa na maafisa wa Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE) wakiwa wamevaa nguo za kiraia alipokuwa akitembea katika kitongoji cha Somerville, Massachusetts.
Mwanafunzi huyo alikaa kizuizini huko Louisiana hadi alipoachiliwa hivi karibuni.
Wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya dhamana Ijumaa, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya, William Sessions, alithibitisha kwamba Ozturk alitoa hoja zinazoridhisha kuhusu ukiukwaji wa katiba katika kesi yake.
Hakimu alisisitiza kwamba kuwekwa kwake kizuizini kimezua wasiwasi mkubwa kuhusu ukiukwaji uhuru, hasa ikizingatiwa kwamba kibali chake cha kuishi kama mwanafunzi nchini Marekani kimebatilishwa kisiasa katika utawala wa Rais Trump.
Utawala wa Rais Trump umefuta visa yake na kuanzisha mchakato wa kumrudisha nyumbani kwa kutegemea makala aliyoiandika akiwa na wenzake kwenye gazeti la wanafunzi la Chuo Kikuu cha Tufts.
Serikali ya Trump imepinga uamuzi wa Jaji Sessions na kuendelea kushikilia msimamo wake kwamba Ozturk anapaswa kutimuliwa Marekani.
Msemaji wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt, alisema Ijumaa kwamba: “Tumeweka wazi kuwa majaji wa vyeo vya chini hawapaswi kuwa na mamlaka ya kuamua sera za kigeni za Marekani na tunaamini kabisa kwamba Rais na Idara ya Usalama wa Nchi wako katika haki zao za kisheria kufukuza wahamiaji haramu.”
Rais wa Marekani aliahidi kufukuza wanaharakati waliojihusisha na maandamano katika kampasi za vyuo vikuu vya Marekani dhidi ya vita vya mauaji ya kimbari vya Israel huko Ukanda wa Gaza.

Chuo Kikuu cha Columbia kimewasimamisha zaidi ya wanafunzi 65 kufuatia maandamano ya kuunga mkono Palestina yaliyojiri katika Maktaba ya Butler ya chuo hicho, alisema afisa wa shule, Ijumaa iliyopita.