"Msingi wa uhusiano wa Russia, Afrika ni mshikamano wa zama za Sovieti"
https://parstoday.ir/sw/news/world-i126640-msingi_wa_uhusiano_wa_russia_afrika_ni_mshikamano_wa_zama_za_sovieti
Russia imesema serikali nyingi za Kiafrika zimedumisha msimamo huru, uliojikita katika kutoingilia kati masuala ya nchi nyingine, kuheshimu mamlaka ya kujitawala na uhuru wa kitaifa, na zimekataa kupasisha vikwazo dhidi ya Russia licha ya mashinikizo makubwa kutoka kwa nchi za Magharibi.
(last modified 2025-05-21T02:26:29+00:00 )
May 21, 2025 02:26 UTC

Russia imesema serikali nyingi za Kiafrika zimedumisha msimamo huru, uliojikita katika kutoingilia kati masuala ya nchi nyingine, kuheshimu mamlaka ya kujitawala na uhuru wa kitaifa, na zimekataa kupasisha vikwazo dhidi ya Russia licha ya mashinikizo makubwa kutoka kwa nchi za Magharibi.

Tatyana Dovgalenko, Mkuu wa Idara ya Ushirikiano na Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema hayo na kuongeza kuwa, nchi za Afrika zimeonyesha uelewa wa wazi wa sababu za mgogoro wa Ukraine na nafasi ya mataifa ya Magharibi katika kuuchochea.

Dovgalenko amesisitiza kuwa, uhusiano wa Russia na Afrika haujaanzishwa hivi karibuni, lakini umekita mizizi kutokana na miongo kadhaa ya urafiki na ushirikiano tangu uungwaji mkono wa Sovieti kwa harakati za ukombozi wakati wa mapmabano dhidi ya wakoloni.

Mbali na kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi na kiusalama baina ya Russia na Afrika, Moscow imeahidi kuzidisha uhusiano na mabadilishano ya kibiashara na nchi za Afrika na kutumia sarafu nyingine badala ya dola katika miamala yao ya kibiashara.

Kwa mujibu wa Dovgalenko, Russia haiitazami Afrika kama uwanja wa ushindani wa kijiografia, lakini kama fursa ya ushirikiano wa kunufaishana.

Amesema mbinu hii inaifanya Russia kuwa tofauti na wachezaji wengine wa kimataifa, kwa sababu Moscow haielezi ni nani mataifa ya Afrika yanafaa kuungana na, wala haiwashinikizi kuegemea upande fulani.

"Tunaheshimu mamlaka yao na maslahi ya kitaifa si kwa maneno, bali kwa vitendo," ameongeza Mkuu wa Idara ya Ushirikiano na Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia.