Afisa wa utawala wa Biden akiri Israel imefanya jinai Ghaza
(last modified Tue, 03 Jun 2025 07:03:49 GMT )
Jun 03, 2025 07:03 UTC
  • Afisa wa utawala wa Biden akiri Israel imefanya jinai Ghaza

Msemaji wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amekiri hadharani kwa kusema: "Ni jambo lisilo na shaka kwamba Israel imefanya jinai ya kivita huko Gaza."

Matthew Miller, msemaji wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani zama za serikali ya Joe Biden ambaye alitumia zaidi ya mwaka mmoja kuhalalisha uungaji mkono usioyumba wa Washington kwa Israel licha ya kuweko ushahidi wa ukiukaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na utawala huo katika Ukanda wa Ghaza, sasa baada ya kuwa hayuko tena serikalini ameiambia televisheni ya Sky News ya Uingereza kwamba, kudai kuwa "swali la je, Israel imefuata siasa za kutenda kwa makusudi jinai za kivita haliwezi kujibiwa, si kweli, swali hilo linaweza kujibiwa."

Msemaji huyo wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema: "Kwa hakika si swali lisiloweza kujibiwa kwani kwa kweli kumekuwa na matukio ya watu binafsi ambayo ni jinai za kivita. Matukio hayo yanaonesha wanajeshi wa Israel na maafisa wa kijeshi wa Israel wamefanya uhalifu wa kivita, na hadi hivi sasa wanajeshi wa Israel hawajawajibishwa kwa matendo yao."

Kwa upande wake, Matt Das, Naibu wa Masuala ya Utendaji wa Kituo cha Utafiti wa Sera za Kimataifa za Marekani amesema: "Rais wa zamani Joe Biden aliwalaghai na kuwadanganya wananchi wa Marekani." 

"Serikali ya Marekani na Congress ziliwapotosha watu wa Marekani kwa sababu Biden alitaka kuendelea kuipa silaha Israel," Das ameandika kwenye mtandao wa kijamii.

Tangu vilipoanza vita mwezi Oktoba 2023 hadi Biden alipoondoka madarakani Januari 20, 2025, utawala wake uliisheheneza Israel silaha za mabalioni ya dola.