UN: Tumesikitishwa mno na vikwazo vya US dhidi ya majaji wa ICC
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk amesema "amesikitishwa sana" na vikwazo vya serikali ya Marekani dhidi ya majaji wanne wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
"Mashambulizi dhidi ya majaji kwa ajili ya utendaji wa kazi zao za mahakama, katika ngazi za kitaifa au kimataifa, yanapingana moja kwa moja na kuheshimu utawala wa sheria na ulinzi sawa wa sheria - maadili ambayo Marekani imesimama kwa muda mrefu," Turk amesema katika taarifa yake ya Ijumaa.
Ametoa wito wa "kuangaliwa upya mara moja na kuondolewa" kwa vikwazo dhidi ya majaji hao, ambao walishiriki katika maamuzi kuhusiana na Afghanistan na Palestina. "Mashambulizi kama haya yanaharibu sana utawala bora na usimamizi unaostahili wa haki," ameongeza afisa huyo wa UN.
Siku ya Alkhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio alitangaza kuwa majaji 4 wa ICC wameongezwa kwenye orodha ya vikwazo, akiwatuhumu kukiuka mamlaka ya Marekani na Israel.
"Watu hawa wanne wameshiriki kikamilifu katika vitendo visivyo halali na visivyo na msingi vya ICC vinavyolenga Marekani au mshirika wetu wa karibu, Israel," Rubio alisema katika taarifa na kuongez kuwa, "ICC ni chombo cha kisiasa na inatumia uwongo kuwachunguza, na kuwashtaki raia wa Marekani na washirika wetu."
Ikumbukwe kuwa, Aprili mwaka huu, watetezi wa haki za binadamu wa Marekani waliwasilisha kesi mahakamani ili kusimamisha amri ya utendaji ya Rais Donald Trump ya kumwekea vikwazo Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Karim Khan, wakisema inakiuka vipengengee vya katiba kuhusu haki zao za uhuru wa kujieleza.