Marekani yajitoa tena katika UNESCO kwa sababu ya Palestina
Marekani imeamua kujiondoa katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa mara ya pili kwa sababu ya uamuzi uliochukuliwa na shirika hilo la UN wa kuikubali Palestina kuwa nchi mwanachama.
Naye msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Tammy Bruce amesisitiza kuwa kubaki katika UNESCO si kwa maslahi ya kitaifa ya Washington, akishutumu shirika hilo kuwa eti lina "ajenda ya kimataifa, ya kiitikadi ya maendeleo ya kimataifa inayokinzana na sera ya kigeni ya Marekani Kwanza".
Ameendelea kueleza kwamba kupokelewa Palestina kama nchi mwanachama na UNESCO kunatazamwa kuwa ni tatizo kubwa na ni kinyume na sera ya Marekani, na hivyo kuchangia kuongezeka utoaji kauli zilizo dhidi ya Israel ndani ya shirika hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema amesikitishwa na uamuzi wa Trump kujiondoa katika shirika hilo, lakini akaongeza kuwa hilo lilitarajiwa, na kwamba UNESCO ilishajitayarisha nalo.
Hatua hiyo ni pigo kwa UNESCO ambayo ilianzishwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia kwa lengo la kuhimiza amani kupitia ushirikiano wa kimataifa katika elimu, sayansi na utamaduni.
Marekani ilijiondoa kwenye UNESCO wakati wa muhula wa kwanza wa Trump lakini ilijiunga tena katika kipindi cha rais wa zamani Joe Biden.../