Tovuti ya data za ujasusi ya CIA yadukuliwa
Wadukuzi wasiojulikana wamedukua tovuti ya Ofisi ya Kitaifa ya Upelelezi ya Marekani (NRO), ambayo hutumiwa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na mashirika mengine ya upelelezi kusimamia kandarasi nyeti na kubadilishana taarifa na makampuni binafsi.
Tovuti hiyo, inayojulikana kama "Acquisition Research Center," ni jukwaa la mawasiliano kati ya mashirika ya kijasusi na makampuni ambayo hutoa teknolojia na huduma zinazohitajika kwa shughuli za kijasusi.
Udukuzi huo umefichua na kuhatarisha maelezo ya umiliki na data ya kibinafsi inayohusiana na programu kadhaa za kina za kijasusi za CIA, ikiwa ni pamoja na programu inayoitwa "Digital Hammer."
Ofisi ya Kitaifa ya Upelelezi ni wakala wa serikali unaohusika na kubuni, kujenga, na kusimamia satelaiti za kijasusi za Marekani, zinazofanya kazi kwa karibu na mashirika kama vile CIA.
Kiwango kamili cha udukuzi huo bado hakijajulikana, lakini vyanzo vinavyofahamu suala hilo vinasema kuwa huenda wadukuzi wamechota teknolojia muhimu inayotumika katika shughuli za CIA.
Mpango wa "Nyundo ya Kidijitali" (Digital Hammer), ambayo ilikuwa moja ya shabaha kuu za udukuzi huo, ni mradi nyeti wa kukuza teknolojia za hali ya juu katika uwanja wa ukusanyaji wa kijasusi wa binadamu, uchunguzi na shughuli za kukabiliana na ujasusi, na umejikita haswa katika kukabiliana na shughuli za kijasusi za China.