Norway: Gaza ni Jahannamu halisi
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway ametaja hali ya maisha katika Ukanda wa Gaza kuwa ni "Jahannamu halisi" na kutoa wito wa kukomeshwa mara moja vita na kuadhibiwa viongozi wa kisiasa na kijeshi wa Israel.
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Åsmund Grøver Aukrust, amesema hali katika eneo la Gaza ni sawa na "Jahannam" na ametoa wito wa kuuchukuliwa hatua za haraka za jamiii ya kimataifa kukomesha maafa hayo na kuwafungulia mashitaka maafisa wa kisiasa na kijeshi wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa mjini The Hague.
Aukrust amesisitiza kuwa hali ya maisha inazidi kuzorota huko Gaza na kusema: "Hali ya sasa ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa siku za nyuma na ni mfano wa ukiukwaji mkubwa zaidi wa sheria za kimataifa."
Norway, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitoa wito wa kukomeshwa mara moja mapigano na kuwezesha kuingia kwa misaada ya kibinadamu huko Gaza, sasa inafanya kazi na nchi kadhaa za Ulaya kuchukua msimamo mkali zaidi wa kuunga mkono usitishaji wa mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway ambaye alitoa matamshi hayo akiwa Afrika Kusini, ameelezea matumaini ya kuongezeka upinzani wa nchi za Ulaya dhidi ya hatua za Israel na kusisitiza kwamba mkutano ujao wa G20 nchini Marekani ni fursa muhimu ya kueleza misimamo thabiti katika suala hili.
Amesisitiza ulazima wa kuwawajibisha maafisa wa kisiasa na kijeshi wa Israel na kuongeza kuwa, Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu mjini The Hague inatarajiwa kutoa uamuzi wa mwisho unaotambua mienendo ya Israel huko Gaza kuwa ni uhalifu wa kivita na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.