Watu milioni 3 wamepoteza maisha kwa kuzama majini duniani muongo uliopita
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO limetangaza kuwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, takriban watu milioni 3 wamepoteza maisha kwa kuzama majini duniani.
Ripoti hiyo imetolewa kwa munasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kuzuia kuzama majini, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Julai. Siku hiyo hutumika kama fursa ya kutafakari juu ya athari kubwa na za kuhuzunisha za kuzama majini kwa familia na jamii, na kutoa suluhisho muhimu za kuzuia vifo vinavyoweza kuzuilika.
Kwa mujibu wa WHO, katika mwaka 2021 pekee, takriban vifo 300,000 vilirekodiwa, ambapo asilimia 12 (takriban 35,000) vilitokea katika Kanda ya Mashariki ya Mediterania. Aghalabu ya wanaozama baharini katika eneo hilo huwa ni wakimbizi Waafrika wanaojaribu kufika Ulaya kinyume cha sheria.
Kanda ya Mashariki ya Mediterania ina kiwango cha pili cha juu zaidi cha vifo vinavyotokana na kuzama kati ya kanda zote za WHO, ambapo vijana na watoto wenye umri wa chini ya miaka 29 wanachangia asilimia 83 ya vifo hivyo. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba, ukanda huo una kiwango cha juu zaidi cha vifo vya kuzama majini kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 4 duniani.
Aidha, ukanda huo umeripoti kupungua kwa kiwango kidogo zaidi cha vifo vinavyotokana na kuzama majini kuliko kanda nyingine, jambo linaloonesha umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti. Kiwango cha juu cha vifo katika nchi za kipato cha chini na cha kati, na pia kiwango cha pili kwa nchi tajiri, ni dalili ya hatari inayowakabili watu wote bila kujali maendeleo ya kiuchumi.
Jinsia, umri, umasikini na ukosefu wa usawa ni sababu kuu zinazoongeza hatari ya kuzama majini. Wanaume wako kwenye hatari mara mbili zaidi ya wanawake. Utafiti unaonesha kuwa wahamiaji, hasa katika Kanda ya Mashariki ya Mediterania, wako kwenye hatari kubwa zaidi. Aidha, takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa watu maskini na waliotengwa kijamii huathirika zaidi – kwa nchi za kipato cha chini, kiwango cha vifo hivyo ni mara 3.2 zaidi ikilinganishwa na nchi tajiri.