Walimwengu waendelea kuandamana kupinga uhalifu wa njaa huko Gaza
Katika kukabiliana na siasa za jinai za utawala wa Kizayuni kwa wananchi wa Palestina, kumefanyika maandamano kadhaa makubwa katika miji mbalimbali duniani.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu huku wakipaza sauti za kuwaunga mkono Wapalestina wamelaani siasa za utawala wa Kizayuni wa Israel za kutumia njaa kama silaha dhidi ya wananchi wa Palestina hususan wa Ukanada wa Gaza.
Mjini New York, Marekani kundi la wanaharakati wa haki za binadamu na haki za kiraia walikusanyika mbele ya ubalozi mdogo wa Israel, wakiwa wameshikilia bendera za Palestina na kupiga nara dhidi ya utwala huo vamizi na ukiukaji wa haki za binadamu, wakitaka kukomeshwa kwa vita na mzingiro dhidi ya Gaza. Waandamanaji hao wamesisitiza juu ya uungaji mkono wa kimataifa kwa wananchi wa Palestina na kuushinikiza utawala unaowakalia kwa mabavu Palestina ukomeshe jinai zake.
Wakati huo huo maelfu ya watu wamekusanyika mjini Geneva Uswisi na kufanya maandamano katika barabara za mji huo kulaani siasa za utawala wa Israel za njaa huko Ghaza. Waandamanaji hao walipiga sahani tupu, wakimaanisha hali mbaya ya njaa na vifo katika Ukanda wa Gaza, na kuimba nara za lugha nyingi, wakiitaka jamii ya kimataifa kuacha kuiunga mkono Tel Aviv na kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Aidha mjini Berlin Ujerumani mamia ya watu waliingia barabarani kuonyesha mshikamano wao na Wapalestina na kulaani sera ya Israel ya mzingiro na njaa dhidi ya Gaza. Wakiwa wameshikilia mabango kama vile "Uhuru kwa Palestina," "Hapana kwa Mauaji ya Kimbari," na "Kimya Chako Chasababisha Mauaji," waandamanaji walifikisha ujumbe wao kwa ulimwengu.