Bunge la Ulaya lataka kutambuliwa rasmi Palestina Huru
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130700-bunge_la_ulaya_lataka_kutambuliwa_rasmi_palestina_huru
Bunge la Ulaya limepasisha azimio likielezea wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya Ukanda wa Gaza, na kuzitaka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuliweka suala la kutambuliwa taifa huru la Palestina kwenye ajenda.
(last modified 2025-09-12T06:37:14+00:00 )
Sep 12, 2025 06:37 UTC
  • Bunge la Ulaya lataka kutambuliwa rasmi Palestina Huru

Bunge la Ulaya limepasisha azimio likielezea wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya Ukanda wa Gaza, na kuzitaka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuliweka suala la kutambuliwa taifa huru la Palestina kwenye ajenda.

Katika kikao cha jana Alkhamisi cha Bunge la Ulaya, azimio hilo lilipitishwa kwa kura 305 za ndio, 151 za hapana na 122 za kujizuia.

Bunge la Ulaya limesema kuwa, haki inayodaiwa ya utawala wa Israel ya kujilinda haiwezi kuhalalisha vitendo vya kijeshi vya kiholela huko Gaza, likielezea wasiwasi wake juu ya uvamizi unaoendelea wa kijeshi na athari zake za kibinadamu.

Azimio hilo la Bunge la Ulaya linaashiria kuweko na mabadiliko makubwa katika uhusiano wa EU na Israel. Aidha linazidisha mashinikizo kwa utawala wa Israel, sambamba na ongezeko la kulaaniwa mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza kote duniani.

Azimio hilo linasisitiza haja ya kufunguliwa mara moja kwa vivuko vya mpaka na kukomesha vikwazo na vizuizi vya kibinadamu dhidi ya Ukanda wa Gaza uliozongirwa. Aidha azimio hilo la Bunge la Ulaya linataka kurejeshwa kikamilifu kwa mamlaka na ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Hali kadhalika, Bunge la Ulaya limesisitizia haja ya kuwekewa vikwazo baadhi ya mawaziri na walowezi wa Kizayuni wa Israel. Nchi za Magharibi zimekuwa kila mara zikitumia lugha tatanishi na ya undumakuwili kuhusiana na Israel na Palestina. 

Hata hivyo weledi wa mambo wanasisitiza kuwa, uamuzi huo wa Bunge la Ulaya ni ujumbe wa wazi kwa utawala wa Kizayuni kwamba, ulimwengu hauko tayari tena kukubali uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu na ukiukaji wa kimfumo wa haki za binadamu.