Deni la umma lailemea serikali ya Marekani, wachumi washikwa na wasiwasi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i132182-deni_la_umma_lailemea_serikali_ya_marekani_wachumi_washikwa_na_wasiwasi
Deni la umma la Marekani limefikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo, ambapo sasa deni hilo linatajwa kufika trilioni 37.9.
(last modified 2025-10-20T05:38:55+00:00 )
Oct 20, 2025 02:35 UTC
  • Deni la umma lailemea serikali ya Marekani, wachumi washikwa na wasiwasi

Deni la umma la Marekani limefikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo, ambapo sasa deni hilo linatajwa kufika trilioni 37.9.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, tovuti ya Economic Times imeandika: Kuongezeka pakubwa deni la umma la Marekani kumewatia wasiwasi wanauchumi, wanasiasa na watu wote wa nchi hiyo. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika kipindi cha mwezi mmoja pekee uliopita, kiwango cha madeni ya Marekani kiliongezeka hadi dola bilioni 400, kiwango ambacho ni sawa na ongezeko la takriban dola bilioni 25 kila siku. 

Hali hii inaakisi changamo za kifedha zinazoitatiza sasa Marekani. 

Tangu kiwango cha deni kilipoongezeka nchini Marekani mwezi Julai mwaka huu; deni la nchi hiyo linatajwa kuongezeka kwa dola trilioni 1.7 hali inayoonyesha kuwa serikali inaendelea kukopa zaidi ili kufidia gharama zake.

Kwa kuzingatia kiwango hicho, weledi wa masuala ya kiuchumi wanatahadharisha kuwa  deni la Marekani linaweza kufikia dola trilioni 40 ifikapo mwaka ujao.

Wakati huo huo, wiwango vya riba ni suala jingine ambalo limezua wasiwasi nchini Marekani. Kwa sasa serikali ya Washington inatumia zaidi ya dola trilioni 1.2 kwa mwaka kama malipo ya riba kwa deni lake, zaidi ya inavyotumia katika masuala ya ulinzi.