Kwa nini China inakosoa hatua za Marekani huko Yemen?
-
China yakosoa vikali hatua za Marekani nchini Yemen
Sun Lei, naibu mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa amepinga madai ya mwenzake wa Marekani katika kikao cha Baraza la Usalama na kusisitiza kuwa: Washington imekiuka sheria za kimataifa kwa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Yemen na kusababisha mateso kwa raia.
Matamshi ya mwanadiplomasia huyo wa China yamekuja kujibu madai ya mwakilishi wa Marekani kwamba baadhi ya zana zinazoitwa za "matumizi mawili" zinazoingizwa Yemen na kutumiwa na majeshi ya nchi hiyo katika mipango ya silaha zina asili ya China.
Naibu mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa akisisitiza msimamo wa wazi wa Beijing alisema: "Siku zote China imekuwa ikichukua tahadhari na kuwajibika kwa mauzo ya bidhaa za kijeshi nje ya nchi na inadhibiti kwa uthabiti usafirishaji wa bidhaa zinazotumika pande mbili zikiwemo ndege zisizo na rubani."
Alisisitiza: "Makampuni ya China yana ushirikiano wa kawaida wa kiuchumi na kibiashara na nchi nyingine, kwa kuzingatia sheria za Shirika la Biashara Duniani na kanuni za soko huria, na haipaswi kulengwa isivyo haki kwa shutuma au mashinikizo."
Msimamo wa China katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambao ni kuepuka kuingiza siasa katika uuzaji nje wa bidhaa zenye matumizi mawili na kutetea ushirikiano halali wa kiuchumi wa makampuni ya China, kwa hakika ni sehemu ya sera ya jumla ya Beijing ya kukataa mashinikizo na shutuma za Washington katika maeneo ya biashara na usalama.
Beijing pia inaamini kuwa Marekani imesababisha mateso na madhara yasiyoweza kufidiwa kwa raia kwa kukiuka sheria za kimataifa kupitia hatua za kijeshi dhidi ya Yemen. Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imekuwa ikishutumiwa kwa kukiuka sheria za kimataifa na kusababisha uharibifu mkubwa wa kibinadamu nchini Yemen kwa kuendesha operesheni za kijeshi za moja kwa moja na kuunga mkono muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.
Ripoti nyingi za Umoja wa Mataifa pia zinaonyesha madhara makubwa kwa raia na mgogoro wa kibinadamu ambao haujawahi kutokea nchini humo.
China imekuwa ikisema mara kwa mara katika vikao vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, mashambulizi ya kijeshi ya Marekani huko Yemen ni kinyume na misingi ya sheria za kimataifa na kwamba mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Yemen hususan dhidi ya ngome za Harakati ya Ansarullah ni ukiukaji wa mamlaka ya kitaifa ya Yemen na misingi ya hati ya Umoja wa Mataifa.
Beijing inasisitiza kwamba, hatua zozote za kijeshi lazima ziidhinishwe na Baraza la Usalama na ndani ya mfumo wa sheria za kimataifa, na zisifanywe kwa upande mmoja na bila uratibu na taasisi za kimataifa. Hii ni katika hali ambayo, operesheni za kijeshi za Washington nchini Yemen zimesababisha mateso na hasara kwa raia na badala ya kupunguza mivutano, zimechochea na kushadidisha mzozo huo.
Ukosoaji wa China dhidi ya Marekani kuhusu kadhia ya Yemen ni mchanganyiko wa wasiwasi wa masuala ya haki za binadamu, maslahi ya kimkakati na ushindani wa kisiasa wa kijiografia.
Nchi hiyo inajaribu kujionyesha kama nguvu inayowajibika na yenye kupenda amani ambayo inaunga mkono utatuzi wa kisiasa kwa migogoro, wakati huo huo ikizingatia hatua za kijeshi za Marekani kuwa zinakiuka sheria za kimataifa na kuzidisha mgogoro wa kibinadamu.
Beijing pia inafanya juhudi kujiimarisha kama nguvu inayowajibika katika uga wa kimataifa. Msimamo huu utasaidia Beijing kuwa na ushawishi zaidi katika Asia Magharibi na kuimarisha nafasi yake katika medani ya kimataifa.
Kwa msimamo huu, Beijing inajaribu kupunguza ushawishi wa Marekani katika kanda hiyo na inajaribu kuonyesha taswira yake ya kupenda amani kama nguvu inayoibukia ya kimataifa.