Aug 16, 2016 15:42 UTC
  • Ban Ki-moon: Atakayechukua nafasi yangu awe mwanamke

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mwanamke ndiye anayepasa kuuongoza Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza tangu ulipoanzishwa zaidi ya miaka 70 iliyopita.

Akiwa anakaribia kumaliza kipindi chake cha pili cha uongozi, Ban amesema ni "wakati mwafaka" kuwa na Katibu Mkuu mwanamke baada ya wanaume wanane mfululizo kuongoza umoja huo.

Kuna wagombea 11 wanaowania kumrithi Ban Ki-moon, sita wakiwa ni wanaume na watano ni wanawake.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa anayemaliza muda wake amesema uamuzi juu ya suala hilo hauko mikononi mwake bali ni wa wanachama 15 wa Baraza la Usalama watakaompendekeza mgombea kwenye Baraza Kuu lenye wanachama 193 kwa ajili ya kuidhinishwa.

Antonio Guterres, ameongoza mara zote mbili katika uchaguzi usio rasmi wa kumpata mrithi wa Ban

Ban amesema kuna viongozi wengi wanawake watajika na wenye kuheshimika walioongoza kitaifa katika serikali, mashirika au jumuiya za kibiashara, kisiasa na kiutamaduni na nyuga nyingine za kimaisha.

Ilivyozoeleka wadhifa wa Ukatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huwa wa mzunguko baina ya maeneo tofauti ya dunia. Shakhsia kutoka Asia, Afrika, Amerika ya Kusini na Ulaya Magharibi wameshashika wadhifa huo.

Mataifa ya Ulaya Mashariki ikiwemo Russia yanasema hayajawahi kutoa Katibu Mkuu na kwamba mara hii ni zamu yao. Wakati huohuo kundi la mataifa 56 linafanya kampeni ya kupata Katibu Mkuu wa kwanza mwanamke wa Umoja wa Mataifa. 

Wanadiplomasia 11 wanaowania Ukatibu Mkuu wa UN

Hadi sasa Baraza la Usalama limeshaitisha zoezi lisilo rasmi la upigaji mara mbili ambapo katika mara zote hizo mgombea mwanamke ameshika nafasi ya tatu. 

Katika mara zote mbili, Antonio Guterres, Waziri Mkuu wa zamani wa Ureno, ambaye amewahi pia kuongoza Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ndiye aliyeshika nafasi ya kwanza.

Baraza la Usalama limepanga kupiga kura tena tarehe 29 mwezi huu na pengine mara moja au mbili tena mnamo mwezi ujao wa Septemba.../

Tags