UN: Marekani kumteka nyara Maduro kunayumbisha usalama wa dunia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135204-un_marekani_kumteka_nyara_maduro_kunayumbisha_usalama_wa_dunia
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeitolea wito jamii ya kimataifa kuwaslisha ujumbe wa wazi kwamba mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa hivi karibuni na Marekani dhidi ya Venezuela, ikiwemo kutekwa nyara Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro, kumeifanya dunia kuwa na usalama mdogo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jan 07, 2026 04:21 UTC
  • Ravina Shamsadani
    Ravina Shamsadani

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeitolea wito jamii ya kimataifa kuwaslisha ujumbe wa wazi kwamba mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa hivi karibuni na Marekani dhidi ya Venezuela, ikiwemo kutekwa nyara Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro, kumeifanya dunia kuwa na usalama mdogo.

Ravina Shamsadani, Msemaji Mkuu wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) amesema mashambulizi ya Marekani dhidi ya Venezuela yanadhoofisha kanuni ya msingi ya sheria za kimataifa. 

Akizungumza mjini Geneva jana Jumanne, Bi Shamsadani amesema: Nchi mbalimbali hazipasi kutoa vitisho au kutumia nguvu dhidi ya mamlaka ya kujitawala au uhuru wa kisiasa wa nchi nyingine. Jamii ya kimataifa inahitaji kuwa kitu kimoja na kutilia mkazo suala hilo. 

Ameonngeza kuwa  uingiliaji kati wa kijeshi unavuruga hali ya usalama wa kimataifa na kufanya kila nchi kutokuwa salama,.

Msemaji Mkuu wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN (OHCHR) amebainisha kuwa kitendo cha aibu kilichofanywa na serikali ya Rais Donald Trump nchini Venezuela "kinatuma ishara kwamba wenye nguvu kubwa wanaweza kufanya lolote wanalopenda."

Bi Shamsadani pia ameashiria wasiwasi wa kimataifa na kusema mustakbali wa Venezuela unapasa kuamuliwa na watu wa nchi hiyo wenyewe. 

Naye Volker Turk Msemaji wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa jana Jumanne alitahadharisha kuwa mashambulizi ya Marekani nchini Venezuela yamedhoofisha kanuni ya msingi ya sheria za kimataifa. 

Jumamosi iliyopita Marekani ilishambulia kambi kubwa zaidi ya kijeshi ya Venezuela katika mji mkuu wa nchi hiyo Caracas, na maeneo ya kimkakati katika majimbo ya Miranda, Aragua, na La Guaira nchini humo.

Wanajeshi wa Marekani walimteka nyara Maduro na mkewe Cilia Flores na kuwasafirisha hadi Marekani kwa ajili ya kushtakiwa kwa madai ya magendo ya mihadarati, kula njama, kuingiza kokaini nchini Marekani na kuvusha silaha. 

Maduro ambaye kwa muda mrefu amekanusha madai hayo, juzi aliiambia mahakama mjini New York kwamba yeye ni mateka wa vita na amekana mashtaka yanayohusiana na dawa za kulevya.