UN yasikitishwa na Trump kuiondoa Marekani katika taasisi za kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135280-un_yasikitishwa_na_trump_kuiondoa_marekani_katika_taasisi_za_kimataifa
Umoja wa Mataifa umesema umesikitishwa na hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump ya kutoa amri ya kuitoa nchi hiyo kwenye taasisi 66 za kimataifa, zikiwemo za UN.
(last modified 2026-01-09T06:43:28+00:00 )
Jan 09, 2026 06:43 UTC
  • UN yasikitishwa na Trump kuiondoa Marekani katika taasisi za kimataifa

Umoja wa Mataifa umesema umesikitishwa na hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump ya kutoa amri ya kuitoa nchi hiyo kwenye taasisi 66 za kimataifa, zikiwemo za UN.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema madai ya Marekani kwamba taasisi hizo za kimataifa yakiwemo mashirika 31 ya Umoja wa Mataifa hazina maana tena na zinaendeshwa ndivyo sivyo haya msingi wowote.

Amesema kujiondoa Marekani kwenye taasisi hizo muhimu za kimataifa kutadhoofisha ushirikiano wa kimataifa na kupunguza uwezo wa taasisi hizo kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Amri hiyo ya Trump ya Januari 7 imevitaka vyombo vyote vya utendani vya Marekani vilivyokuwa vinadhamini fedha za taasisi 31 za Umoja wa Mataifa na 35 zisizo za Umoja wa Mataifa ziache mara moja kudhamini fedha hizo.

Hiyo ni hatua ya hivi karibuni zaidi kuchukuliwa na Trump ya kuitoa Marekani kwenye taasisi za kimataifa. Huko nyuma serikali ya Marekani ilikuwa imeacha kusaidia taasisi nyingine za kimataifa kama vile Shirika la Afya Duniani WHO, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwasaidia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). 

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, hatua hiyo mpya ya Trump itazidi kupunguza imani ya mataifa ya dunia kwa Marekani na kuongeza ushawishi wa wapinzani wake wakuu kama China na Russia katika majukwaa ya kimataifa.