Ujumbe wa safari ya Rais Putin nchini China kwa ulimwengu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i138530-ujumbe_wa_safari_ya_rais_putin_nchini_china_kwa_ulimwengu
Siku nne tu baada ya kufanyika safari ya Rais Donald Trump wa Marekani nchini China, Rais Xi Jinping wa nchi hiyo amemkaribisha kwa shangwe Rais Vladimir Putin wa Russia mjini Beijing.
(last modified 2026-05-21T13:36:45+00:00 )
May 21, 2026 13:34 UTC
  • Ujumbe wa safari ya Rais Putin nchini China kwa ulimwengu

Siku nne tu baada ya kufanyika safari ya Rais Donald Trump wa Marekani nchini China, Rais Xi Jinping wa nchi hiyo amemkaribisha kwa shangwe Rais Vladimir Putin wa Russia mjini Beijing.

Safari za Donald Trump na Vladimir Putin nchini China ndani ya wiki moja zimezingatiwa na duru za kisiasa na vyombo vya habari kuhusu nafasi ya Beijing katika muundo mpya wa nguvu duniani. Vyombo vya habari vya serikali ya China vimeelezea muda mfupi kati ya safari za viongozi wa Marekani na Russia nchini humo kama ishara ya nafasi muhimu iliyonayo Beijing kama "kitovu cha diplomasia ya kimataifa."

Jarida la Newsweek la Marekanbi limeandika kwamba Putin, ambaye awali alimwita Xi "rafiki mpendwa," amepata matokeo mazuri zaidi kuliko yale aliyoyapata Trump katika mkutano wake na rais wa China. Philippe Lecour, mhadhiri wa mahusiano ya kimataifa na masuala ya Asia katika chuo cha biashara cha ESSEC nchini Ufaransa, anaamini kwamba muda wa safari ulichaguliwa kwa umakini mkubwa na kutuma ujumbe wa wazi kuhusu vipaumbele vya kimkakati vya China. Anasema kwamba, Beijing inajaribu kuonyesha kuwa washirika wake wa karibu ni Russia, Iran na Korea Kaskazini, nchi ambazo huhudhuria hafla muhimu za China.

Zhichun Zhou, mkurugenzi wa Taasisi ya China katika Chuo Kikuu cha Bucknell huko Marekani, anaamini kwamba safari ya Putin mjini Beijing mara tu baada ya safari ya Trump inatuma ujumbe muhimu kwa nchi za Magharibi, hasa Marekani, kuwa Putin ana uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa Xi. Kulingana na Zhou, wakati ulimwengu mzima umeelelekeza macho yake katika matukio ya Lango-Bahari la Hormuz, safari ya Putin huko Beijing ni ukumbusho kwamba vita vya Ukraine bado vinaendelea na kwamba utatuzi wa kidiplomasia ni muhimu. Xi ameweza pia kumwonyesha Trump kuwa ana kadi nyingi za kijiopolitiki mikononi mwake.

Beijing inajaribu kuonyesha kuwa ni nguvu kubwa inayotegemewa katika ulimwengu unaotikiswa na mivutano ya kibiashara, vita na migogoro ya nishati. Hii ni safari ya 25 ya rais wa Russia nchini China, ambapo maafisa kutoka nchi zote mbili wanaziona kama ishara ya ushirikiano mkubwa wa nchi hizo katika nyanya zote. Muungano huu unazidi kuimarika wakati ambao miji mikuu ya nchi za Magharibi imeitaka China mara kwa mara kutumia uwezo na ushawishi wake kusimamisha vita vya Russia nchini Ukraine. Katika ngazi ya kisiasa, Beijing inajidhihirisha kama mpatanishi wa amani na mchezaji asiyeegemea upande wowote. Hii ni katika hali ambayo Putin ameweka wazi kwamba miundo ya madaraka nchini China na Russia inaunga mkono na kutetea kikamilifu maslahi ya kimsingi ya pande zote mbili.

Russia, ikiwa chini ya vikwazo vya Magharibi, inatafuta mikataba mipya ya nishati kutoka kwa uchumi wa pili kwa ukubwa duniani ili kudhamini mahitaji ya kifedha ya serikali ya Moscow na jeshi la Russia katika vita vya Ukraine. Ian Storey, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Yusuf Ishak huko Singapore, amesema kuwa mkutano wa viongozi hao wawili unatuma ujumbe wa wazi kwa ulimwengu kwamba ushirikiano wa kimkakati kati ya Moscow na Beijing ni msingi wa sera za kigeni za nchi mbili. Amesisitiza kuwa jaribio lolote la Marekani la kuleta mifarakano kati yazo halitafanikiwa.

Putin ametia saini hati ishirini katika nyanja mbalimbali wakati wa safari yake ya siku mbili nchini China. Uhusiano wa Russia na China umeongezeka tangu kuanza kwa vita vya Ukraine mnamo Februari 2022. Katika miaka minne iliyopita, China imeagiza mafuta ya dola bilioni 370 kutoka Russia. Karibu asilimia sabini ya biashara ya Russia inafanyika nchini China. Ingawa biashara hii kubwa imeifanya Russia kutegemea China kama taifa kuu la kiuchumi na kijeshi, lakini imeipa uwezo wa kustahimili vikwazo vikali vya Magharibi na kuiwezesha kugharamia vita vya Ukraine. Beijing na Moscow zinazidi kukurubiana kimaoni na kimsimamo kuhusu milinganyo ya kisiasa, kiusalama na nishati duniani.

Kwa upande mwingine, sera za kivita, upendeleo, ubaguzi na uchokozi za Trump zimedhoofisha uhusiano wa Marekani na nchi nyingi duniani katika pande mbili za Bahari ya Atlantiki. Hakuna serikali yoyote ya Ulaya na washirika wa Marekani barani Asia ambao wanaafikiana na sera za Washington katika kuizingira Iran baharini. Katika miaka themanini ya ushirikiano wa kimkakati kati ya Marekani na Ulaya katika muungano wa kijeshi, NATO, muungano huo haujawahi kulegalega na kutokuwa na utulivu kama ilivyo sasa. Kadiri kwamba Friedrich Mertz, Kansela wa Ujerumani na mmoja wa wanasiasa wakuu wa kihafidhina barani Ulaya wanaounga mkono Marekani, amezungumzia suala la kufikia kikomo "Ndoto ya Marekani" na ardhi ya fursa. Amesema hawashauri tena watoto wake kwenda Marekani kwa ajili ya masomo au kufanya kazi.

Ulimwengu uko katika mabadiliko ya kihistoria. Uvamizi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeharakisha mchakato huu wa mpito. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa na taathira kubwa katika uga wa kieneo na kimataifa kwa kupinga na kukabiliana kishujaa na uvamizi huu wa Marekani na utawala wa Kizayuni. China na Russia pia zimetumia fursa hii kusimama na Iran.