Utafiti: Wamarekani waliowengi wanataka vita dhidi ya Iran visitishwe haraka
https://parstoday.ir/sw/news/world-i138906-utafiti_wamarekani_waliowengi_wanataka_vita_dhidi_ya_iran_visitishwe_haraka
Takribani Wamarekani saba kati ya kumi wanautaka utawala wa nchi hiyo ukomeshe vita vyake visivyo halali dhidi ya Iran “haraka iwezekanavyo.” Hayo ni kwa mujibu wa utafiti mpya uliofichua kiwango kikubwa cha kutoridhika kwa umma kuhusu mashambulizi ya kijeshi ya utawala wa Trump ambayo yanaendelea kwa zaidi ya miezi mitatu.
(last modified 2026-06-05T12:44:38+00:00 )
Jun 05, 2026 10:56 UTC
  •  Utafiti: Wamarekani waliowengi wanataka vita dhidi ya Iran visitishwe haraka

Takribani Wamarekani saba kati ya kumi wanautaka utawala wa nchi hiyo ukomeshe vita vyake visivyo halali dhidi ya Iran “haraka iwezekanavyo.” Hayo ni kwa mujibu wa utafiti mpya uliofichua kiwango kikubwa cha kutoridhika kwa umma kuhusu mashambulizi ya kijeshi ya utawala wa Trump ambayo yanaendelea kwa zaidi ya miezi mitatu.

Utafiti wa The Economist/YouGov umeonyesha kuwa asilimia 68 ya waliohojiwa wanaamini kuwa Marekani “inapaswa kufikia makubaliano ya kumaliza vita nchini Iran haraka iwezekanavyo.”

Matokeo haya yanaangazia kuongezeka upinzani ndani ya Marekani dhidi ya vita hivyo vya gharama kubwa na vinavyosababisha misukosuko, ambavyo vimeweka mzigo mkubwa kwa uchumi wa dunia na kudhoofisha sana hadhi ya Marekani katika medani ya kimataifa.

Kufungwa Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani, kufuatia uchokozi ulioanzishwa na Marekani dhidi ya Iran, kumesababisha kupanda kwa kasi bei za nishati katika sehemu mbalimbali za dunia.

Familia za kawaida za Wamarekani sasa zinahisi moja kwa moja athari za kiuchumi za uchokozi wa hatari wa utawala wa Trump uliotekelezwa kwa maslahi ya Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Siku ya Jumatano, Baraza la Wawakilishi la Marekani lilipitisha hatua inayolenga kumlazimisha Rais Donald Trump kusitisha vita dhidi ya Iran.

Muswada huo ulipitishwa kwa kura nyembamba ya 215 dhidi ya 208, ambapo wajumbe wanne wa chama tawala cha Republican walijiunga na chama cha upinzani cha Democrats kuunga mkono sheria hiyo.

Matakwa makubwa ya Wamarekani ya kuona vita vinamalizika haraka yanaakisi uchovu uliosambaa miongoni mwao kutokana na kuendelea sera za kivita za utawala wa Trump.

Kwa upande wake, Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kujitolea kwake kwa ajili ya amani na utulivu wa kikanda, sambamba na haki yake ya kujilinda dhidi ya mchokozi yeyote.

Wakati uchumi wa Marekani ukiendelea kulemewa na mzigo wa vita hivyo, shinikizo linaongezeka kwa utawala wa Trump kuheshimu matakwa ya wananchi wa Marekani na kukomesha mara moja vita vyake visivyo halali dhidi ya Iran.