Korea Kaskazini: Tumejiandaa kutoa jibu kali kwa chokochoko za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i15424-korea_kaskazini_tumejiandaa_kutoa_jibu_kali_kwa_chokochoko_za_marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini amesema kuwa, nchi yake imejiandaa kutoa jibu kali kwa vitisho vya Marekani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 16, 2016 07:42 UTC
  • Korea Kaskazini: Tumejiandaa kutoa jibu kali kwa chokochoko za Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini amesema kuwa, nchi yake imejiandaa kutoa jibu kali kwa vitisho vya Marekani.

Ri Yong Ho ameyasema hayo nchini Venezuela ambako amesafiri kwa ajili ya kushiriki kikao cha nchi zisizofungamana na siasa za upande wowote ambapo sanjari na kuashiria hatua za kichochezi za Marekani katika peninsula ya Korea, amesema kuwa, nchi yake imejiandaa vyema kutoa jibu kali kwa mienendo hiyo ya Washington katika eneo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini amesisitiza kuwa, raia wa Korea Kaskazini wameazimia kutoa jibu kwa uchokozi wowote wa Marekani dhidi yao.

Jaribio la kombora la nyuklia la Korea Kaskazini

Siku chache zilizopita, serikali ya Pyongyang ilifanya jaribio la tano la kombora la nyuklia na kutangaza kuwa kombora hilo lina uwezo wa kubeba kichwa cha nyuklia. Baada ya jaribio hilo, ndege mbili za kivita za Marekani zilipaa kwenye anga ya Korea Kusini. kitendo ambacho kimetajwa na Korea Kaskazini kama cha kichokozi. Jaribio la Korea Kaskazini, limezifanya nchi za Kimagharibi, hususan Marekani na Ufaransa, kutaka kushadidishwa vikwazo zaidi dhidi ya Korea Kaskazini katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.