Waislamu wa Austria walalamikia mpango wa kuwazuia kuvaa Hijabu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i23017-waislamu_wa_austria_walalamikia_mpango_wa_kuwazuia_kuvaa_hijabu
Waislamu wa nchi Austria wamelalamikia vikali mpango wa kuwapiga marufuku kuvaa vazi la staha la Hijabu katika maeneo ya kazi za umma.
(last modified 2026-01-02T07:57:23+00:00 )
Jan 07, 2017 15:57 UTC
  • Waislamu wa nchini Austria
    Waislamu wa nchini Austria

Waislamu wa nchi Austria wamelalamikia vikali mpango wa kuwapiga marufuku kuvaa vazi la staha la Hijabu katika maeneo ya kazi za umma.

Shirika la habari la Fars limeripoti leo Jumamosi kwamba, Waislamu wa Austria wamemtaka Sebastian Kurz, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kufanya mazungumzo nao, kuhusiana na marufuku hiyo katika maeneo ya umma.

Omral Rawi, mkuu wa jopo kuu taasisi ya Waislamu wa Austria amesema, serikali na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, bila ya shaka wanahitajia uungaji mkono wa Waislamu.

Naye mshauri wa serikali ya Austria na baadhi ya weledi wa mambo wamependekeza kuwa, kuna wajibu wa kujadiliwa kwa kina marufuku hiyo ya Hijabu kabla ya kuingizwa katika sheria.

Sebastian Kurz, Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria alitangaza kuwa, serikali ya nchi hiyo ina nia ya kuwapiga marufuku Waislamu kuvaa vazi la staha la Hijabu katika maeneo ya umma wakiwemo walimu mashuleni.

Hivi sasa chama cha kihafidhina cha Austria kinaandaa muswada wa kuifanya marufuku hiyo kuwa sheria. Iwapo muswada huo utapitishwa na bunge la nchi hiyo, Waislamu watazidi kunyanyaswa katika nchi hiyo ya Ulaya.

Mwaka 2011 nchi nyingine ya Ulaya yaani Ufaransa ilipiga marufuku vazi la staha la Hijabu. Nacho chama cha kihafidhina pamoja na watu wenye misimamo mikali ndani ya chama tawala nchini Ujerumaini wameitaka nchi hiyo ipige marufuku burqa.